Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais
Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw.
Charles Kitwanga umefuata kanuni za utumishi wa umma ambao unakataza mtumishi
kulewa akiwa kazini.
“Zipo sheria za utumishi ambazo mtumishi
hatakiwi kunywa pombe na wala hapaswi kulewa akiwa kazini… mtumishi anapaswa
kuwa na akili timamu inayokuwezesha kufanya kazi za Serikali,” alisema.
Ametoa ufafanuzi leo
usiku (Ijumaa, Mei 20, 2016) wakati akijibu swali la mwandishi wa TBC1
aliyetaka kujua kama taarifa zilizoenea kuhusu kutenguliwa kwa Waziri huyo ni
za kweli.
“Ni kweli Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe
Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Charles
Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei, 2016 baada ya kuonekana amelewa wakati wa
kazi. Na hili lilibainika pale alipokuwa akijibu maswali ya wizara yake leo
asubuhi,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema
kuna swali aliloulizwa ambalo hakulijibu vizuri na kwamba swali hilo litapaswa
kurudiwa kuulizwa baada ya wabunge kuomba muongozo wa swali hilo.
IMETOLEWA NA: OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, MEI 20, 2016
No comments:
Post a Comment