Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara
moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo
na abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
(Terminal One) Dar es salaam.
Rais Magufuli ametoa
agizo hilo leo tarehe 13 Mei, 2016 alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja
huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo
hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maafisa wa uwanja wa
ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa wakitoa maelezo juu ya
hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa
wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi,
hali iliyosababisha Dkt. Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana
na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri
uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza? eeeh sasa
sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya
kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima,
akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi
miwili."Dkt. Magufuli aliwahoji Maafisa wa uwanja wa
ndege
“Kwa hiyo mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile,
kwa hiyo mtu nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu,
na almasi zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu” Rais Magufuli aliendelea kuwabana
maafisa hao wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Rais Dkt. John Pombe
Magufuli amefanya ziara hii ya kushtukiza mara baada ya kuwasili katika uwanja
wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Jijini Kampala nchini Uganda ambako
jana alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri
Kaguta Museveni.
No comments:
Post a Comment