Hospitali ya Rufaa ya
Amana, Ilala imewasimamisha kazi madaktari wawili na muuguzi mmoja, kwa madai
ya kumtolea lugha isiyostahili mjamzito Asha Said (17), aliyejifungulia chooni.
Tukio hilo lilitokea
mwezi uliopita katika hospitali hiyo, baada ya Asha kujifungulia chooni na
madaktari na wauguzi hao kumtolea lugha chafu, bila kuelezwa sababu za kufanya
hivyo.
Mganga Mkuu wa Amana,
Dk Meshack Shimwela alisema jana kwamba watumishi hao ambao hakuwataja
wamepelekwa katika Baraza la Watumishi na Madaktari la hospitali hiyo kwa
uchunguzi zaidi.
“Kilichotokea siku ile ni kauli zilizotoka kwa watumishi hao kwenda kwa
mama aliyejifungua, ambaye pia alikuwa mdogo kiumri.
“Sisi madaktari na waaguzi tuna taratibu za kinidhamu, huwa tunazifuata
baada ya watumishi kubainika kufanya makosa, hatua ya kwanza ndiyo hiyo
tusubiri nyingine wakati uchunguzi ukiendelea dhidi yao,” alisema Dk Shimwela.
Dk Shimwela ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), alisema kilichohitajika ni
lugha nzuri kwa sababu kisheria ni lazima kwa mgonjwa yeyote kuoga akifika
hospitali, ili kumkinga na maradhi mbalimbali.
Wakati hayo yakitokea
Amana, Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kimeitaka jamii kuendelea kuibua
matukio ya unyanyasaji na huduma mbaya wanazofanyiwa na wakunga wakati wa
kujifungua, ili vyombo vinavyohusika viweze kuliona tatizo kwa ukubwa wake na
kulifanyia kazi.
Akizungumza katika
kongamano la siku mbili la kujadili maendeleo ya wakunga nchini, rais wa chama
hicho, Feddy Mwanga alisema kila wanaposikia malalamiko kuhusiana na
unyanyasaji na huduma mbaya kwa wajawazito, chama hicho hufanya utafiti na
kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.
No comments:
Post a Comment