Shehena ya sukari ya kilo milioni 34 zilizokuwa zimefichwa kwenye
maghala ya wafanyabiashara watatu Kilimanjaro imekamatwa na vyombo vya usalama,
na serikali mkoani humo imetangaza kuiuza kwa wananchi kuanzia jana kwa bei
elekezi ya Sh. 1,800.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecki Sadiki alithibitisha
jana kukamatwa kwa shehena hiyo, baada ya makachero wanaoongoza timu maalumu ya
ukaguzi wa maghala ya wafanyabiashara na mawakala wa sukari kubaini kufichwa
kwa bidhaa hiyo.
“Tumefanya ukaguzi
katika maghala 45 na katika harakati hizo tumenasa kilo milioni 34 za sukari
iliyokuwa imefichwa," alisema.
"Katika zoezi
hilo kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa, yeye alikutwa na tani 31.33 lakini
alikuwa akiiuza, isipokuwa bado tumewapa kazi Mamlaka ya Mapato (TRA) ichunguze
kama imehodhiwa isivyo halali,”alisema Sadiki.
Kiasi cha sukari iliyobakia, alisema Mkuu wa M koa huyo,
kilikamatwa kwa wafanyabiashara wengine wawili, ambao walikuwa na tani nne
kasoro, Moshi mjini na Marangu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, shehena hiyo ya sukari hadi
jana mchana ilikuwa ikishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukamilisha
taratibu za kiuchunguzi na kwamba ametoa amri igawiwe kwa wananchi kwa bei
elekezi iliyotangazwa na serikali.
Kuhusu upungufu wa sukari Kilimanjaro, Sadiki alisema "Sisi kama mkoa tumefanya mawasiliano na mawakala
walioko Dar es salaam, ambao sukari yao ilikuwa inashikiliwa na vyombo vya
usalama na wametuahidi kuukabili uhaba wa sukari uliopo hapa kwetu.
“Jana (juzi)
niliwasiliana na Mmiliki wa Kampuni ya Zakaria Enterprises na amekubali kuwapa
bidhaa hiyo mawakala ambao ni wadau wa Kiwanda cha Sukari cha TPC," alisema Sadiki.
"Kwa hiyo
tunakwenda vizuri na tumejipanga kuhakikisha kwamba uhaba huo tunaupatia
ufumbuzi wa kudumu.Ila ninawaomba wananchi wangu wawe wavumilivu kwa sasa.
"Mawakala wakubwa
wa sukari wa Kilimanjaro na mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni mfanyabiashara
Vicent Laswai ambaye atapatiwa tani 600 za sukari kutoka Kampuni ya
Zakaria, alisema Mkuu wa Mkoa
huyo.
Aidha, Laswai atapokea tani 640 toka katika Kampuni ya Mohamed
Enterprises, alisema.
Kampuni ya Zakaria pia imekubali kutoa tani 640 kwa Kampuni ya
Marenga Investment, alisema Sadiki na kubainisha kuwa Mohamed Enterprises
imemuahidi kuziba pengo la upungufu utakaojitokeza.
Tangu Rais Magufuli apige marufuku uingizaji sukari kutoka nje
ya nchi Februari 17 mwaka huu, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu
wamekuwa wakificha bidha hiyo kama njia ya kuihadaa serikali kwamba kuna uhaba
mkubwa.
Wakati akipiga marufuku, Magufuli alisema kama kutakuwa na
uhitaji wa sukari kuingia nchini, vibali atavitoa yeye si mtu mwingine yeyote
ili kuviwezesha viwanda vya ndani viendelee kuzalisha bidhaa hiyo, kuendelea
kutoa ajira na kuinua kipato cha wakulima wa miwa.
Alisema inasikitisha kuona sukari ikiingizwa nchini kutoka nje
wakati nchi ina viwanda vingi vya bidhaa hiyo na kusababisha Watanzania wengi
kupoteza ajira kutokana na sukari wanayozalisha kukosa soko.
"Nakuagiza Waziri
Mkuu, kuanzia leo, marufuku mtendaji yeyote wa Serikali kutoa kibali cha
kuagiza na kuingiza sukari kutoka nje ya nchi...vibali vyote nitatoa
mimi," alisema Rais Magufuli.
"Katika kampeni
zangu mwaka 2015, nilisema Serikali yangu itakuwa ya viwanda hivyo lazima
tuvithamini viwanda vya ndani na kulinda bidhaa zinazozalishwa."
No comments:
Post a Comment