Kwa miaka kadhaa sasa kilimo kimekuwa na mchango mkubwa katika
uchumi wa Tanzania hasa katika upatikanaji wa chakula, biashara ya mazao nje ya
nchi, kusaidia upatiakaji wa malighafi za viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa
Watanzania.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2015 Tanzania iliuza jumla ya
tani 125,134 za mazao ya kilimo katika soko la nje ikiwemo tani 63,237 za
mahindi, Ngano tani 42,538, Mpunga Tani 7,651 na Mihogo Tani 11,708.
Pamoja na kwamba zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania watagemea
kilimo na kutoa zaidi ya asilimia 65 ya malighafi kwa ajili ya viwanda nchini,
asilimia kubwa ya shughuli za kilimo zinafanywa na wakulima wadogo.
Hata hivyo pamoja na umuhimu na sekta ya kilimo kwenye uchumi wa
nchi, bado ukuaji wa sekta hiyo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali
kama vile kiwango kidogo cha uzalishaji, ukosefu wa mbinu na teknolojia za
kisasa, matumizi madogo ya umwagiliaji, ukosefu wa mtaji na ukosefu wa mikopo
kwa wakulima.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa
ni jitihada za Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo nchini.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa benki hiyo Dkt. Jakaya Kikwete
alisema kuwa Serikali imekuwa ikisaidia sekta ya kilimo kupitia ruzuku za
pembejeo na mbolea na kwa sasa imeanzisha benki ili kero mbalimbali za wakulima
zitatuliwe kwa wakati.
Pia Dkt. Kikwete aliwataka wakulima kutambua kuwa kilimo ni
shughuli inayoweza kuwaletea kipato kikubwa, hivyo watutumie fursa zinazotolewa
na Benki ya Kilimo katika kuendeleza sekta hiyo na kujiongezea zaidi kipato
kwani ni wakati kwa wakulima kufanya shughuli hiyo kiutaalamu zaidi badala ya
kuendelea na kilimo cha mazoea.
Mbali na kutekeleza sera ya Serikali kuhusu upatikanaji wa fedha
za kuendeleza kilimo, pia benki ya kilimo imepanga kusaidia upatikanaji wa
utoshelezi na usalama wa chakula utakaokuwa endelevu na kusaidia kuleta
mapinduzi ya kilimo ili kuwatoa watanzania katika kilimo cha mazoea kwenda
katika kilimo cha kibiashara.
Katika kutimiza lengo la kuanzishwa kwake
Benki ya kilimo imetoa elimu kwa wakulima ambapo vikundi 89 vyenye
Wakulima 21,526 vilipatiwa elimu mkoani Iringa, kufanya tafiti mbalimbali
kwenye sekta ya kilimo, kuwajengea uwezo wakulima hasa vijana katika kuanzisha
miradi ya kilimo ili pale watakopewa mikopo waweze kuitumia vizuri na kuwaletea
faida katika shughuli zao.
Benki imejipanga kutoa mikopo ya mudamfupi,
(Hadi Miaka 2); muda wa kati (zaidi ya miaka 2 hadimiaka 5); na muda mrefu
(zaidi ya miaka 5 hadimiaka 15) kwa Wakulima wadogowadogo, wa kati na wakubwa
ili kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani
katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugajinyuki).
Akiongea na waandishi wa habari Mkurugenzi
Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Bw. Thomas Samkyi alisema Benki
hiyo imejipanga kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwa
riba nafuu (kati ya 7% hadi 12%) kwa kupitia muungano wa vikundi vya
Wakulima wadogo wadogo, benki za maendeleo ya jamii, vyama vya kuweka na
kukopa, taasisi ndogo za fedha, vyama vya ushirika na taasisi au vyama vya
wakulima.
Bw. Semkyi aliongeza kuwa benki hiyo imetoa
mikopo kwa wakulima kwa kwa vikundi 8 vya wakulima wapatao 857 na sasa
inashughulikia maombi ya mikopo kwa awamu nyingine yenye thamani ya Zaidi ya Sh
Bilioni 40.
“Napenda kuwashauri wakulima wajiunge katika
vikundi ili kuirahisishia benki kuwatambua na kutoa mikopo ya riba nafuu ya
kati ya asilimia 7 hadi 12 ili waweze kuendesha shughuli zao za kilimo katika
maeneo ya uzalishaji mazao, uvuvi na ufugaji hali itakayowawezesha kuwatoa
katika kufanya kilimo cha mazoea na kwenda katika kilimo cha kibiashara”
Alisema Bw. Semkyi.
Akifafanua kuhusu aina ya riba hasa kwa
vikundi, Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa Benki ya Kilimo
Bw.Robert Paschal alisema kuwa Riba yake ni asilimia saba hadi nane
na wanaokopeshwa ni wakulima wadogo walio kwenye vikundi.
Alisema wakulima hao watapata mkopo kwa ajili
ya ununuzi wa mbegu bora, kulima shamba na mahitaji mengine ya shamba ambapo
marejesho ya mkopo huo ni mara baada ya mkulima kuvuna mazao.
Bw. Paschal aliongeza kuwa kama msimu wa
mavuno haukuwa mzuri, labda mvua hazikunyesha na mkulima hawakupata mavuno,
wakijiridhisha na ukweli wa hilo, mkopo unasogezwa msimu unaofuata.
Aidha Bw. Paschal alisema kuwa aina
nyingine ya mkopo ni wa kati, unaotozwa kwa kipindi cha miaka miwili hadi
mitano na riba yake ni asilimia tisa hadi 10, na mkopo huo ni kwa ajili ya
kusaidia ununuzi wa vifaa vya kilimo na upanuzi wa mashamba.
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata baada ya
kupata mkopo kutoka TADB, kiongozi wa Chama cha Nzihi Mixed Crops kilichopo
Mkoani Iringa Bw. Emmanuel Fungo anasema benki hiyo imewapatia mkopo wa
shilingi Milioni 222 ambao umewasaidia sana kwa sababu wameupata kwa
muda walioutarajia na bila masharti magumu tofauti na taasisi nyingine
zinazolazimu kuhamishia akaunti yako kwenye taasisi hiyo.
Anasema sanjari na kuwapatia mkopo huo pia
TADB imewatafutia mteja wa mazao (Mahindi) watakayozalisha hivyo wana uhakika
watauza mazao na kuweza kulipa mkopo na kubaki na mazao ya ziada.
Rai yangu kwa wakulima ambao mara nyingi
wamekuwa wakilalamikia uhaba wa rasilimali fedha katika kuendeleza shughuli zao
za kilimo ni kutumia fursa inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania.
Alisema benki hiyo imejiwekea malengo katika utoaji
mikopo ya uongezaji wa thamani katika shughuli za kilimo na kuwawezesha
wakulima kupata masoko ya uhakika wa mazao wakati wa mavuno.
No comments:
Post a Comment