Kadri siku ya kuzima simu feki kote nchini inavyokaribia imebainika kuwa
wanaozitumia wanazidi kupungua nchini.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy amesema tangu ilipotangaza mwaka
jana kuwa itazima simu feki ifikapo mwishoni mwa Juni, idadi ya watumiaji
imepungua kutoka asilimia 30 hadi 13.
Alisema wakati wa uhakiki wa matumizi ya simu feki Desemba mwaka
jana, mamlaka hiyo ilibaini kuwapo asilimia 30 ya simu bandia zinatotumika
nchini.
TCRA ilifanya uhakiki mwingine Februari ambao ulibaini matumizi
ya simu feki kupungua hadi asilimia 18.
“Uhakiki wa Machi
ulibaini matumizi yameshuka zaidi hadi kufikia asilimia 13,” alisema Mungy na kubainisha kuwa TCRA
itafanya tathmini nyingine kabla ya muda kumalizika.
“Tunatumaini matumizi ya
simu feki yataendelea kupungua. Hadi kufikia Juni mwishoni kusiwe na mtu
anayetumia simu feki,” alisema Mungy.
Meneja huyo alisema matokeo ya tathmini hizo ni kinyume na
matarajio yao.
“Watu wameonyesha mwitikio mzuri. Wengi wameacha kuzitumia kabla
hatujazizima,” alisema.
Alisema wananchi wamekuwa na mwitikio huo kwa sababu mamlaka
hiyo imekuwa ikitoa elimu kote nchini juu ya matumizi ya simu hizo.
Hadi sasa, TCRA imeshatoa elimu kuhusu wananchi kuacha kutumia
simu feki, katika Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati na
wiki ijayo mamlaka hiyo itakuwa Kanda ya Ziwa.
Alisema elimu hiyo pia itatolewa kwa wananchi wa mikoa ya Pwani,
Morogoro, Lindi na Mtwara.
Alisema Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa simu
feki utakuwa wa mwisho kupatiwa elimu hiyo, Juni kabla ya kuzima simu hizo.
Kuhusu watu wanaoweka namba feki za utambulisho (IMEI) kwenye
vifaa vya elektroniki, alisema wanafanya kazi bure kwa sababu hata hizo
zitazimwa siku ikifika.
“Mitambo yetu ina
uwezo wa kugundua namba za IMEI halisi na feki,”alisema Mungy.
Alisema hata mtu akibadilisha namba ya IMEI halisi kwenye siku
feki, siku ya kuzima simu feki itazima tu.
Pia, alisema ni vigumu kuwagundua watu wanaofanya ujanja huo kwa
sababu wanapokuwa wanazibadilisha simu inakuwa imezimwa.
No comments:
Post a Comment