Mkazi wa Kitongoji cha
Kapembo, Kijiji cha King’wangoko wilayani Kaliua, Mkoa wa Tabora, ametiwa
mbaroni akituhumiwa kumuua, mama yake mzazi , Kiziko Lukambwe kwa
kumnyonga kisha kumtundika ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Tabora, Hamis Issa alisema kijana huyo anatuhumiwa kumnyonga mama yake na
kumning’iniza ndani ya nyumba, ili ichukuliwe kuwa amejinyonga.
Issa alieleza kuwa
uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwamba, polisi
wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi.
Alionya wanaofanya
uhalifu hawatapata nafasi ya kukimbia mkono wa sheria.
Majirani wa Kiziko,
walieleza kwamba mwanamke huyo amekuwa akilalamika kuwa haelewani na mtoto
wake.
“Kiziko inaelekea hakuwa na uhusiano mzuri na mwanaye kwa vile alikuwa
akilalamika kuwa, hawaelewani,” alisema mkazi wa Kona nne, Yuda Ngati.
Wilaya ya Kaliua ina
matukio mengi ya mauaji yatokanayo na sababu mbalimbali, ikiwamo ulipizaji
visasi na imani za ushirikina.
Kamanda Issa aliwataka
wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kwamba, Serikali haitawavumilia
watu wa aina hiyo.
Pia, alitaka kamati za
ulinzi na usalama za vijiji kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na askari na
kwamba, polisi peke yao hawawezi.
No comments:
Post a Comment