Wakati viongozi
wakiendeleza kasi ya Rais John Magufuli ya utumbuaji wa majipu, Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wanaoiga kasi hiyo kutenda haki, ikiwamo
kufuata taratibu na sheria.
Akizungumza kwenye
maadhimisho Siku ya Wauguzi Duniani mkoani Geita jana, Samia aliwataka viongozi
na wanasiasa kufuata taratibu za kazi, ikiwamo kutoa nafasi ya kujitetea kwa
watumishi wanaotuhumiwa.
Alitoa kauli hiyo, baada
ya wauguzi kulalamika kwenye hotuba yao kwamba kuna viongozi waliwatumbua
wauguzi bila kuwatendea haki.
“Hata hivyo, nakiomba Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), kuweka
utaratibu wa kufuatilia maadili ya wauguzi na kuwachukulia hatua za kisheria,
wale wote ambao wanakwenda kinyume na kiapo chao cha kazi,” alisema.
Rais wa Tanna, Magesa
Paul alimuomba Makamu wa Rais kutembelea maeneo yao ya kazi, ili ajionee hali
halisi ya wauguzi wanavyofanyakazi katika mazingira magumu, ikiwamo kukosa
vitendea kazi na nyumba za kuishi.
Jijini Dar es Salaam,
mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliwataka
wauguzi kuhakikisha wanatii maadili ya kazi, bila hofu ya kupigiwa simu na
baadhi ya viongozi wa Serikali waliozoea kutaka upendeleo wa huduma, kinyume na
maadili yao.
“Tunaomba wauguzi mkitendee haki kiapo chenu cha kazi, na mtumie siku
hii muhimu kuutathmini utendaji wenu wa kazi katika kuwasaidia wananchi,” alisema.
Alisema Serikali
inatambua changamoto za wauguzi, hivyo wasitumie matatizo yao katika
kuwanyanyasa wagonjwa, bali wawasaidie na kuwaonyesha upendo.
Akisoma risala kwa
niaba ya wauguzi wenzake, muuguzi wa Hospitali ya Temeke, John Mgonja alilaani
tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kutumia madaraka kuvuruga utaratibu wa
muda wa kuwaona wagonjwa.
“Bila kujali muda uliowekwa wa kuwaona wagonjwa, baadhi ya viongozi
hutaka kuingia kuwaona wagonjwa wao kutokana na madaraka waliyo nayo, bila
kujali kuwa kufanya hivyo kunachelewesha huduma,” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa,
Musa Wambura aliwaomba wauguzi kuhakikisha wanafanya kazi kwa umakini na
weledi, ili kuepusha lawama kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment