Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emmanuel Mjema akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) inayoonesha kuwa chuo hicho kimepata ziada ya bilioni 1.2 kati ya mwaka huu na kufanya chuo kujiendesha kwa faida tofauti na baadhi taarifa za upotoshaji zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari.
Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) kimewataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji
zilizoripotiwa
na Baadhi ya vyombo vya Habari Hapa nchini kuhusu chuo hicho.
Akizungumza na vyombo vya Habari leo jijini Dar es
salaam Mkuu wa chuo hicho Prof. Emmanuel Mjema amesema tuhuma za kuwa chuo hicho kina ubadhirifu wa kutisha si
za kweli na zinalenga kuchafua taswira ya chuo hicho.
“Chuo kinafanyiwa ukaguzi wa Hesabu zake na Mkaguzi
na Mdhibiti wa hesabu za Serikali na kwa kipindi cha miaka minne tumepata hati
safi (clean audit report) kuanzia mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015 .” alisisitiza
Prof. Mjema.
Katika ukaguzi huo ripoti hiyo ilionyesha kuwa
Taasisi hiyo imekuwa ikizingatia sheria na kanuni za matumizi ya fedha za umma
hali iliyopelekea kupata hati safi kwa kipindi chote.
Pia Chuo hicho kilifanyiwa ukaguzi na Mamlaka ya
Udhibiti wa manunuzi Serikalini (PPRA) kwa mwaka unaoishia 2014/2015 na Chuo
hicho kupata alama 95.8 hivyo kuwa moja ya Taasisi za Umma zinazofanya vizuri
katika kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi ya umma.
Prof. Mjema amesema kuwa chuo hicho kimekuwa
kikijiendesha bila kupata ruzuku toka Serikalini na pia kuzalisha mapato ya
ziada zaidi ya bilioni moja kwa kwa kila mwaka wa fedha kuanzia mwaka 2013 hadi
2015.
Kutokana na Mafanikio hayo chuo hicho kimeweza
kuanzisha Kampasi ya Mbeya ambapo chuo hicho kimenunua eneo lenye ukubwa wa
ekari 54.9 na pia maboresho katika maktaba ya chuo yamefanyika.
Mkuu wa Chuo cha Elimu Biashara (CBE) Prof. Emmanuel Mjema akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya Mwaka huu inayoonesha chuo hicho ni moja kati ya Taasisi 14 zilizofanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 95.8 katika kufuatilia sheria ya manunuzi ya umma na kuutaka umma kupuuza taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa wanakiuka sheria hizo.
No comments:
Post a Comment