Walimu 35,411 nchini
wataajiriwa katika shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha
2016/2017.
Watakaokaidi kwenda
kuripoti katika mikoa ya pembezoni, hawataajiriwa na serikali.
Hatua hiyo imeelezwa
kwamba imetokana na serikali kupokea maombi mengi ya kazi kwa walimu, ambao
mwaka jana hawakuripoti katika vituo walivyopangiwa pembezoni mwa miji kwa
kutegemea kuajiriwa na shule binafsi, lakini hawakufanikiwa.
Naibu Waziri wa Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema hayo alipokuwa
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) aliyetaka
kufahamu serikali inafanya nini kwa walimu waliopangiwa kwenda mikoa ya
pembezoni, ikiwemo Lindi na kwingineko, lakini hawakuripoti.
Jaffo alisema ni kweli
kuna walimu wengi ambao hawakuripoti katika mikoa ya pembezoni. Alisema si
Lindi peke yake, bali na mikoa mingine, ikiwemo Katavi na Kigoma.
Alisema kwa mwaka huu,
wataajiri walimu 35,411, lakini ambaye hataripoti katika mikoa hiyo na kuishia
mijini tu, hawataajiriwa tena serikalini, kama wanavyoomba tena baada ya kukosa
katika shule binafsi.
No comments:
Post a Comment