Siku chache baada ya
watu saba wa familia moja kuuawa kwa mapanga wilayani Sengerema mkoani Mwanza,
polisi wamefanikiwa kuwatia mbaroni watu 12 kwa tuhuma za mauaji hayo huku
mmojawapo akikamatwa kwa mganga wa kienyeji alikokuwa akijitibu.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema hadi jana upelelezi wa tukio hilo lililozua
hofu kwa wakazi wa Kijiji cha Sima unaendelea na tayari watuhumiwa 12
wamekamatwa.
“Hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa katika
upelelezi wa jambo hili, tutawasaka na kuwakamata wote waliohusika kwa njia
moja au nyingine na mauaji haya ya kinyama,” alisema Msangi.
Habari zilizopatikana
kutoka kwa mtu wa karibu na familia ya marehemu Zakaria Mbata iliyopoteza mama
na watoto watatu katika tukio hilo, zinaeleza kuwa wauaji walilenga kupora
fedha zilizohifadhiwa kwenye mtandao wa simu.
Pia, chanzo kimoja cha
habari kilisema kuwa polisi walimkamata mmoja wa watuhumiwa hao akiwa kwa
mganga wa kienyeji alikokuwa akijitibu jeraha alilopata siku ya tukio.
“Katika purukushani za mauaji hayo, huyo mhalifu alijeruhiwa usoni,
inaonekana alipigwa na kitu kizito, akakutwa kwa mganga wa kienyeji na
amekamatwa kwa mahojiano,” kilisema chanzo hicho
Tukio la mauaji hayo
lilitokea usiku wa kuamkia Mei 11, watu wasiojulikana walivamia familia ya
Zakaria Mbata na kuua watu saba kwa kuwakata mapanga sehemu mbalimbali za
mwili.
Waliouawa katika tukio
hilo ni mama wa familia hiyo, Augenia Philipo (62), mdogo wake Maria Philipo
(56) na watoto wake; Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12) na Mkiwa Philipo
(13).
Wageni wawili wa
familia hiyo, waliojulikana kwa jina mojamoja ya Donald na Samson nao pia
waliuawa katika tukio hilo.
No comments:
Post a Comment