Kesho Mei 28
katika dimba la San Siro, kutakuwa na pambano kali la fainali ya UEFA pale Real
Madrid watakapokuwa wakichuana na mahasimu wao wakubwa Atletico Madrid. Hii
imekuwa ni fursa adhimu sana kwa makocha wa timu zote mbili yaani Zinedine
Zidane na Diego Simeone kuoneshana umwamba kutokana na wote kuwa na historia ya
kuvichezea vilabu hivyo.
Kwa kufahamu
umuhimu wa pambano hili, tumeamua kukuletea baadhi ya mambo muhimu ya
kukumbukwa kati ya makocha hawa hawa kuelekea pambano hili;
·
Diego Pablo Simeone (El Cholo) amewahi kuitumikia Atletico
Madrid kama mchezaji katika vipindi viwili tofauti (1994-97 na 2003-05).
·
Zinedine Zidane alijiunga na Real Madrid kama mchezaji katika
dirisha kubwa la usajili la majira ya joto mwaka 2001 na kudumu kwa miaka
mitano mpaka msimu wa mwaka 2005-06 alipoamua kustaafu soka.
·
Zidane aliichezea Real almaarufu Blancos michezo 227, akifunga
mabao 49 na kubeba makombe sita ,likiwemo la UEFA ambapo alifunga goli la
kipekee baada ya kupiga mpira aina ya ‘volley’ katika fainali dhidi ya Bayer
Leverkusen ya Ujerumani mwaka 2002.
·
Simeone alikuwemo ndani ya kikosi cha kukumbukwa cha Atletico
kilichochukua kwa pamoja La Liga na Copa del Rey mwaka1996. Tangu achukue
mikoba ya kuwa kocha amefanikiwa kubeba makombe matano na kuongeza idadi ya
makombe katika klabu hiyo – La Liga, Copa del Rey, Supercopa mawili na ligi ya
Europa.
·
Derby ya kwanza ya Zidane ilikuwa ni Januari mwaka 2003 pale
timu hizo zilipotoshana nguvu kwa kufungana magoli 2-2.
·
Kipigo kikubwa cha Simeone akiwa kama mchezaji wa Atletico
kilikuwa ni Desemba mwaka 1994 ambapo Atletico walifungwa mabao 4-2.
·
Desemba 3, 2003, Zidane na Simeone walikutana kama wachezaji wa
Real na Atletico katika dimba la Santiago Bernabeu. Magoli ya Ronaldo de Lima
na Raul Gonzalez yalihitimisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Atletico Madrid.
·
Machi 4, 2006, Zizou alicheza mechi yake ya mwisho dhidi ya
Atletico. Katika mchezo huo Real Madrid walishinda mabao 2-1.
·
Baada ya kushindwa kuwaonesha umwamba Real Madrid wakati
akiichezea Atletico, akiwa kama kocha Simeone amebadili kabisa upepo wa
Atletico, amekuwa akiifunga Real kadri anavyojisikia.
·
Mchezo wa kwanza kwa Zidane kama kocha mkuu wa Real Madrid
ulikuwa dhidi ya Deportivo la Coruna.
·
Kipigo cha mabao 4-1 Atletico walichokipata dhidi ya Real, ndiyo
ilikuwa ‘derby’ ya kwanza kwa Simeone akiwa kama kocha. Mchezo huo ulipigwa
April 2012 katika dimba la Vicente Calderon.
·
Zidane, alionja ladha ya ubingwa akiwa kama kocha msaidizi wa
Carlo Ancelotti mwaka 2014 katika fainali ya UEFA baada ya Real Madrid kuinyuka
Atletico mabao 4-1. Mchezo huo ulipigwa Lisbon Ureno.
·
El Cholo amewahi kuchukua makombe mbele ya Real Madrid wakati wa
fainali. Amechukua Copa del Rey na Supercopa.
·
Derby ya kwanza ya Zidane akiwa kama kocha alipokea kipigo cha
bao 1-0 katika dimba la Santiago Bernabeu, moja kati ya mchezo wa ovyo
alioshuhudia timu yake ikicheza tangu alipoanza kuifundisha Real.
Na hatimaye
sasa, Zidane na Simeone wanakutano kesho katika fainali ya UEFA wote wakitaka
kulipiza kisasi kwa namna ya tofauti. El Cholo akitaka kulipiza machungu ya kipigo
cha mwaka 2014 cha magoli 4-1 kutoka kwa Real, wakati Zidane kuonesha umwamba
akiwa kama kocha Mkuu wa Madrid katika fainali yake ya kwanza na kuwapa ubingwa
baada ya kufanya hivyo mwaka 2014 akiwa kama kocha msaidizi.
Yote kwa yote,
hii inatarajiwa kuwa ni fainali ya aina yake kutokana na makocha wote wawili
kufahamiana vilivyo ndani na nje ya uwanja. Diego Simeone akitegemea hamasa,
ari na nguvu kutoka kwa wachezaji kuipa ushindi timu yake, huku Zidane
akitegemea zaidi ubora wa mastaa wake kama Ronaldo na Bale ili kuamua matokeo
ya mchezo.
Yetu macho,
kesho ndiyo kesho ama El Cholo au Zizzou, atakayechanga karata zake vizuri
ndiye ataibuka mshindi na kutwaa ndoo ya UEFA kwa mara ya kwanza katika
historia zao za maisha yao ya ukocha.
No comments:
Post a Comment