Taasisi ya kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) imebaini kuwepo kwa sukari
iliyofichwa tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kwa mujibu wa Taarifa
iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentine
Mlolowa Taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo
imefafanua kuwa mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala
yaliyopo Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.
TAKUKURU tayari
imetembelea Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni
mwa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha
bidhaa hiyo.
Aidha uchunguzi
uliofanywa na Taasisi hiyo ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza
sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani
hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji wa
sukari hiyo ili iweze kusambazwa.
Taarifa hiyo
imeendelea kufafanua kuwa katika eneo la Kitumbini kumekuwa na wananchi
wengi wanaohitaji bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa
licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
Katika uchunguzi wake
TAKUKURU pia imebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na
mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha
kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku
wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari
katika soko.
Kuficha bidhaa ni kosa
la uhujumu uchumi na ni kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya
Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali haitavumilia
hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote
ataekwenda kinyume na sheria hii.
TAKUKURU inatoa
wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na
vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya
hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
No comments:
Post a Comment