Friday, 20 May 2016

JESHI LA POLISI JIJINI DAR ES SALAAM LAFANIKIWA KUMKAMATA TAPELI WA MADINI


Kamanda wa Polisi kanda maaalum ya Dar es Salaam Kamishna Simon Sirro akionesha waandishi wa habari mzani unaodaiwa kutumiwa na tapeli wa madini kupima madini bandia na kuwatapeli wananchi wakati wa kutoa taarifa ya kukamatwa kwa tapeli huyo Jijini Dar es salaam Mei 20 2016.



Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata mtuhumiwa anayejulika kwa jina la Wenceslaus Mtui(46) mkazi wa Makongo Juu kwa kosa la utapeli wa sh. Milioni 90.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi kanda maaalum ya Dar es Salaam Kamishna Simon Sirro amesema wamefanikiwa kumkamata tapeli huyo mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa Bw. Kelvin Nyerere(26) mkazi wa Msasani ambaye alishawishiwa na kutapeliwa kwa kuuziwa madini bandia na mtuhumiwa huyo.

Kwa mujibu wa kamanda Sirro, mtuhumiwa huyo alikamatwa mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa Nyerere aliyetapeliwa, askari walifika eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa  na kumfikisha kituo cha polisi kwa mahojiano.

Aidha baada ya kufanyika kwa upekuzi ofisini na nyumbani kwa mtuhumiwa, kulikutwa na vitu vilivyodhaniwa kuwa ni madini, chuma cha kuchomea madini, mashine ya kupimia madini, vifaa vya kubania madini (53), mashine ya kupimia madini, nyaraka za kuwekea fedha kutoka Benki mbalimbali na hati za usajili wa makampuni ambazo zilitiliwa shaka.Vielelezo vyote vilichukuliwa kwa uchunguzi.

Mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi upepelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili za kufanya utapeli wa kuuza madini bandia ambayo ni kinyume cha Sheria za nchi.

Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu wanaojifanya wafanyabiashara wa madini kuacha mara moja tabia hiyo na wananchi wanaohitaji kununua madini wafike Ofisi za Wakala wa Madini(TMAA) ili kuepukana na matapeli.



No comments:

Post a Comment