Maji
ni rasilimali muhimu kwa maisha ya viumbe vyote pamoja na maendeleo ya kiuchumi
na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote, ubora wa afya na mazingira
kwa ujumla vinategemea kuwepo kwa maji yakutosha na yenye ubora unaotakiwa.
Maji
yana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya jamii kwa kuwa hutumika kwa
matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha umeme,kupika, kuoga na kufua nguo,
katika ujenzi na kusaidia maisha ya viumbe hai, matumizi ya viwandani pamoja na
kilimo hivyo usimamizi na utunzaji wake lazima uzingatiwe.
Serikali
ina malengo ya kuwapatia maji wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani,
Kibaha pamoja na Bagamoyo kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.
Hakika
aja ya mja hunena, muungwana ni vitendo. Hii imethibitika kuwa kweli Serikali
ya Awamu ya Tano inajali watu wake hasa wa hali ya chini kama Rais John Pombe
Magufuli ambavyo hupenda kuwaita wanyonge. Watu wengi wanahitaji kuwa na maji
ya bomba lakini uwezo wa kuunganisha ulikuwa mgumu kwani gharama wengi waliiona
kuwa ni kubwa sana. Kwa kulitambua hilo Serikali imeamua kuingia gharama za
kuwaunganishia maji wateja wake na wenyewe watalipia kidogo kidogo gharama
hizo. Hili ni jambo la kuungwa mkono sana.
Hapa
tunamsikia mkazi wa Mbweni, Jijini Dar es Salaam, Bi Fatuma Iddi akisema,“Kwa
kweli serikali hii imetukumbuka, mimi nilishapoteza matumaini ya kupata maji
kwangu kwani sikuwa na uwezo wa kulipa malaki hayo kwa ajili ya kuunganishiwa.
Lakini kwa kulipia kwa awamu hilo nitalimudu. Heko Mhe. Rais Magufuli kwa
kutujali hasa sisi wanyonge.”
Takwimu
zilizotolewa na Ofisi ya Mkoa wa Dar es Saalam zinaeleza kuwa Mkoa unapata maji
kutoka katika mito na visima ambapo eneo kubwa la Mji huo linahudumiwa na
Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka
ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA) na kwa maeneo yasiyo na
mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka kwenye visima vinavyoendeshwa na vyombo
vya watu binafsi.
Aidha,
vyanzo vikuu vya maji yanayopatikana katika Mji wa Dar es Salaam ni mitambo ya
Ruvu Juu ambao kwa siku unazalisha jumla ya lita milioni 82, Ruvu Chini
unazalisha lita milioni 270, Mtoni unazalisha lita milioni 9 na visima virefu
106 ambavyo vinazalisha jumla ya lita milioni 106 kwa siku.
Vyanzo
vyote hivi huzalisha wastani wa jumla ya lita milioni 371 kwa siku
zinazotosheleza asilimia 75 ya mahitaji ya wananchi.Mahitaji ya maji kwa Mkoa
wa Dar es Salaam yamefikia Lita milioni 450 kwa siku yakijumuisha matumizi ya
nyumbani, matumizi ya Viwanda, Kilimo, Mifugo, na usafi wa Jiji kwa siku.
Hata
hivyo mtandao wa DAWASA unapoteza takribani Lita 128,000 sawa na asilimia 48
kwa siku kutokana na ubovu wa mitambo, uchakavu wa mabomba na matumizi yasiyo
halali lakini hali hii inaendelea kudhibitiwa na DAWASA kwa kukarabati
miundombinu yake, kuwawekea wateja mita za kupima kiasi cha maji wanayotumia,
kuelimisha wananchi na kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaopatikana na
makosa ya uharibifu wa miundombinu au wizi wa maji, kuongeza matanki ya
kuhifadhia maji na kufunga mabomba mapya kwenda maeneo yasiyokuwa na huduma na
kuchimba visima virefu.
Hii
inaonyesha dhahiri kuwa maji yanayozalishwa bado hayatoshelezi wakazi wa Mji
huu lakini Serikali inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wananchi wake
kuondokana na adha hii ya ukosefu wa maji safi na salama.
Katika
kutekeleza kauli mbiu ya “Hapa kazi tu” ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kuwa ifikapo Juni mwaka huu
wateja 400,000 wa Mkoani Dar es Salaam wawe wamepatiwa huduma ya maji safi na
salama.
Ili
kutekeleza agizo hilo, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam imeamua
kugharamia uunganishaji wa huduma hiyo kwa wakazi wake ambapo gharama hiyo
ilikua ikilipwa na mteja mwenyewe.
Mtendaji
Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, Mhandisi Cyprian
Luhemeja amesema kuwa zoezi hili la kugharamia uunganishaji wa huduma ya maji
kwa wateja ni kwa kipindi maalumu cha miezi miwili ambayo ni Mei na Juni ambapo
mteja atawajibika kurudisha gharama za uunganishaji kidogo kidogo kila mwezi kwa
muda wa miezi kumi na mbili.
“Fursa
hii itasaidia hata kwa wananchi wenye kipato cha chini kuweza kuunganishiwa
huduma ya maji hivyo nawasihi wananchi wa sehemu husika kujitokeza kwa wingi
kupatiwa huduma hii,”alisema Mhandisi Luhemeja.
Naye
Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni hiyo Bi. Everada Balati ametoa rai kwa
wananchi kutopuuzia fursa hii kama walivyopuuzia fursa zingine zilizopita kwa
kuwa hii ni ya tofauti na anaamini kuwa watu wengi wataweza kuimudu.
“Huduma
hii ni ya haraka kwakua haichukui zaidi ya wiki kukamilika,mteja wetu atalipia
kulingana na urefu wa sehemu ambayo atafikishiwa huduma hiyo”,alisema Bi.
Balati.
Bi.
Balati amesisitiza kuwa malipo haya hayatakuwa na riba bali mteja atahitajika
kulipia gharama za uvutaji wa bomba kama zilivyoainishwa na utaratibu wa malipo
utaunganishwa pamoja na bili ya kawaida ya maji inayopelekwa kwa mteja kila
mwezi.
Wakazi
wa Dar wanashauriwa kuitumia fursa hii nzuri iliyotolewa na DAWASCO ili kuweza
kupata huduma ya maji safi kwa urahisi kwa kuwa gharama za uunganishwaji
zilikua zikiwashinda wananchi wengi sasa unaunganishiwa na kulipia gharama hizo
kidogo kidogo kwa muda wa miezi 12.
Kusema
ukweli hii ni fursa kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani na imekuja kipindi
muafaka ambapo mtambo mkubwa wa maji wa Bagamoyo unakaribia kuanza rasmi. Hii
itaondoa adha ya wakazi wa jiji ambao walilazimika kuamka usiku wa manane ili
kupata maji pindi yanapotolewa kwa mgao. Pia itaondoa kero ya kuuziwa maji
yasiyo salama ambayo watu wengi wamekuwa wakinunua bila kujua maji hayo
yanapatikana wapi na yako safi na salama kiasi gani.
Falsafa
au kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu imetafsiriwa kwa vitendo. Hii inajibu kauli mbiu
jingine iliyokuwa inasema Maisha Bora kwa kila mtanzania. Haya kwa hakika
yatakuwa maisha bora kwa kila mtanzania kwani hakuna ambaye siku hupia bila
kutumia maji, iwe mtoto, mkubwa na hata kikongwe anahitaji maji. Ndio maana
watu husema ya kuwa Maji ni Uhai.
DAWASCO
zoezi hili mlikamilishe kwa wakati kama mnavyosema kuwa litadumu kwa miezi
miwili yaani Mei na Juni. Uondoaji wa kero ya maji utasaidia nguvu nyingine na
muda uliokuwa unatumika kwa ajili ya kutafuta maji, kutumika kwa shughuli
nyingine za uzalishaji mali.
No comments:
Post a Comment