Polisi mkoani Mara
inamshikilia mganga wa zahanati katika Kijiji cha Rwamchanga
wilayani Serengeti kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito
aliyejifungua pacha na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mara, Ramadhan Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Mei 15.
“Tunamshikilia kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi
na kushindwa kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, tunaendelea na mahojiano
yatakapokamilika atafikishwa mahakamani,”alisema Ng’anzi.
Akisimulia chanzo cha
mwanae kupoteza maisha, Shida Mugesi akiwa katika Hospitali ya Nyerere alisema
alifika zahanati saa 12 asubuhi na kumuomba mganga amuhudumie, lakini alikataa.
“Nilikaa kwa muda wa saa mbili bila kupatiwa huduma, ghafla nilihisi
uchungu wa kusukuma mtoto tukamuita mganga wa zamu ili anisaidie aligoma na
kudai nimsubiri anakwenda kuoga na wakati huo alikuwa anazungumza kwa simu bila
kuonyesha ushirikiano. Nilianza kujifungua mwenyewe,” alisema.
Muuguzi ambaye
hakutaka jina lake litajwe alisema walipopima uzito wa watoto kwa mjamzito huyo
walibaini kuwa aliyefariki alikuwa na kilo 2.5 na mwingine 2.3.
Muuguzi wa zahanati
hiyo, Frida Kasonga alisema aliposikia taarifa ya kuwapo kwa mgonjwa huyo
alilazimika kurudi kituoni kumsaidia lakini alikuta mtoto mmoja ameshafariki
dunia.
“Haikuwa zamu yangu ila nililazimika kurudi baada ya kusikia mganga
aliyekuwa zamu kagoma kuwasaidia,” alisema Frida.
Ofisa mtendaji kata,
Fadhila Nyamburapi na Mwenyekiti wa kitogoji cha Kazi, Samwel Nyakande
walilaani kitendo hicho na kutaka sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment