Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona akiongea
na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la siku 60
kwa wadaiwa wa Bodi hiyo na waajiri, ambapo takribani asilimia 72 ya wadaiwa
wote wameshawasilisha taarifa zao. Kulia ni Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano
wa Bodi hiyo.
Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kushoto) akieleza
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusu utaratibu wa urejeshaji wa mikopo kwa wadaiwa ambao mikopo yao
imeshaiva. Kulia ni Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona
Jumla ya wadaiwa wapya 21,721 wa mikopo ya elimu ya juu
wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao kufuatia agizo la siku 60
lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mnamo Machi
14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
Bw. Robert Kibona wakati akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu tathmini ya agizo
lililotolewa na bodi hiyo kwa wanufaika
wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw. Kibona alifafanua kuwa jumla ya Shilingi bilioni
151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao walikopeshwa ili kuwawezesha
kupata elimu yao ya juu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuanzia
mwaka 1994.
“Lengo la agizo lilikuwa ni kuhahakisha
madeni yote yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania
wengi zaidi na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka huu.” alisema Bw. Kibona
Kwa
mujibu wa Bw. Kibona, kati ya wadaiwa waliopatikana, wadaiwa 19,528
walipatikana baada ya Bodi kuchambua taarifa za waajiriwa zilizowasilishwa na
waajiiri na wadaiwa wengine wapatao 2,007 walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri
wana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao
walifanya hivyo katika siku hizo sitini na tukawabaini wadaiwa hao,
tunawapongeza waajiri kwa ushirikiano walioutoa na wanufaika wote waliojitokeza
kwa hiari” alisema Bw. Kibona.
Aidha Bw. Kibona aliongeza kuwa Bodi imeongeza
siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa wadaiwa waliobaki kujitokeza na
uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri
na wanufaika wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas Mwaisobwa
alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi kinatarajiwa kuongezeka
kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi sasa na kufikia shilingi
bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.
Katika kipindi cha
mwaka 1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa
wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hivi sasa ambao
kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale watakapomaliza au kusitisha masomo
yao.
No comments:
Post a Comment