Serikali imefanikiwa kuwezesha vikundi 1200 vya wakulima wadogo
wadogo nchini ili kupata masoko ya uhakika ya mazao yao wanayozalisha.
Akizungumza kuhusu mradi wa kuboresha miundombinu ya
masoko,uongezaji wa thamani na huduma za kifedha vijijini (MIVARF) Mratibu wa
Taifa wa Mradi huo Bw. Walter Swai amesema malengo ya mradi huo ni kuongeza
kipato cha wakulima na uhakika wa chakula kwa kutengeneza miundombinu ya
upatikanaji wa masoko kwa wakulima kwa kuboresha barabara za kutoka mashambani
kuelekea sokoni na kuwapa taarifa sahihi kuhusu masoko na mahitaji yake.
Bw Walter Swai ameongeza kuwa lengo la mradi ni kufikia vikundi
1,600 kwa nchi nzima katika kutoa elimu ya kuwezesha wakulima kupata masoko ya
mazao yao ikiwa ni jitihada za Serikali kuwawezesha wakulima hao kujikwamua
kiuchumi.
“Nia yetu ni kufikia vikundi 1,600 katika mikoa yote Tanzania
Bara na Visiwani na hadi sasa tumefika asilimia 75 ya lengo tulilojiwekea la
kuwawezesha wakulima wadogo kupata masoko ya mazao yao” alisema Bw.Swai.
Naye Mtaalamu wa Masoko ya mazao ya kilimo wa MIVARF Bw. Muhoni
Leonard amesema kuwa mradi huo utasaidia kuwapa wakulima taarifa sahihi juu ya
masoko na mahitaji yake na kupunguza gharama ambazo zilikuwa zinatumika kwa
ajili ya kupata taarifa hizo kutoka kwa madalali.
“Azma ya mradi huu ni kubadili muundo na utendaji wa wakulima
wadogo kuongeza ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji wa masoko ya mazao
husika” alisistiza Bw Leonard.
Aidha, mmoja wa wakulima na msindikaji wa mchele kutoka Wilaya
ya Chato mkoani Geita Bw.Joseph Nchimani amesema kuwa elimu aliyoipata kutoka
MIVARF imemuwezesha kuendesha kilimo cha mpunga kwa njia ya kisasa ambayo imemuwezesha
kuongeza thamani ya mchele kwa kuufunga kwenye mifuko iliyo katika hali ya
ubora unaokubalika kwenye soko.
“Kabla ya kuanza kufunga mchele kwenye mifuko nilikuwa nauza
jumla ya tani mbili mpaka kumi kwa mwaka ila baada ya MIVARF kuja na kunipa
elimu hii nimeweza kuuza mpaka kufikia tani 50 kwa mwaka” alisistiza
Bw.Nchimani.
Program hiyo ya MIVARF
inajushughulisha pia na kutoa huduma za kifedha vijijini ambayo ni ya miaka
saba inayotekelezwa kwa mikoa 30 ya Tanzania Bara na Visiwani na inasimamiwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment