Watu sita wanaodaiwa kumbaka na
kumlawiti msichana kisha kumrekodi na kusambaza video hiyo, leo wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni pamoja na Iddi Adamu Mabena (32) Mkazi wa
Njombe na Zuberi Thabiti (30) Mkazi wa Mbalali, Mbeya ambapo kesi
hiyo inasimamiwa na waendesha mashtaka watatu wa serikali- Grolia
Rwakibalila, Edgar Bantulaki na Kalistus Kapinga.Akisoma maelezo ya kosa katika shtaka la kwanza la kubaka na kulawiti, Wakili Rwakibalila aliwataja wahusika kuwa ni pamoja na Iddi Adamu na Zuberi Thabiti.
Mwendesha mashataka huyo amedai kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja huku wakijua kufanya hivyo ni kosa, walimbaka na kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 21 na kumsababishia maumivu makali.
Wakili huyo alidai kuwa, washtakiwa hao walimbaka na kumuingilia kinyume na maumbile msichana huyo tarehe 27 Aprili, saa 1 usiku katika nyumba ya kulala wageni ya Titii iliyopo katika Tarafa ya Dakawa Wilaya ya Mvomero.
Hata hivyo, mawakili wote wa serikali walipinga dhamana ya washtakiwa hao kwa madai kuwa, kesi hiyo imegusa hisia za watu wengi hivyo kwa usalama wao pia kuhofia kuharibu ushahidi ni bora waendelee kushikiliwa.
Mbele ya Marry Moyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi washtakiwa hao walikana kuhusika na mashtaka hayo ambapo wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Juni Mosi mwaka huu na kwamba, upelelezi haujakamilika.
Katika shtaka la pili washtakiwa hao wakiwa na wenzao wanne walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kusambaza picha chafu za ngono katika mtandao wa kijamii wa whatsapp.
Edgar Bantulaki, mwendesha mashataka amedai kuwa, washtakiwa hao wamefanya kosa hilo chini ya kifungu cha sheria namba14 (1) (b) na 2 (b) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Bantulaki amewataja washtakiwa wengine kuwa ni pamoja na mshtakiwa namba 1 na 2 na Rajabu Salehe, (30), Ramadhani Ally (26), Muhsin Ng’ahy (36), John Peter (24) wote wakiwa ni wakazi wa Wami, Dakawa wilayani Mvomero.
Mwendesha mashtaka huyo amedai kuwa, washtakiwa wote kwa pamoja walianza kusambaza picha hizo kati tarehe 28 hadi 30 Aprili mwaka huu wilayani Mvomero na mkoa mzima wa Morogoro kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp.
Hata hivyo Ignas Kunge, wakili wa mshtakiwa wa nne (Ally) aliiomba mahakama kumpa dhamana mshtakiwa wake jambo lililopingwa na mawakili wa serikali kwasababu suala hilo limegusa jamii zaidi pia kwasababu za kutoingilia na kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Ivan Msaki, washtakiwa hao walikana kuhusika na shtaka hilo ambapo wamerejeshwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Juni Mosi mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kujadiliwa suala la dhamana iliyopingwa kwa kiapo na mawakili wa serikali.
Urlich Matei, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amesema, washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani kati ya 11 waliokuwa wakituhumiwa kuhusika na tuhuma hizo kufuatia upelelezi kutokamilika dhidi yao.
Kamanda Matei amesema, katika hatua za awali upelelezi kipolisi ulikamilika kwa watuhumiwa sita wa mwanzo ambao ndio wamefikishwa mahakamani.
Aidha amesema kuwa, vitendo vilivyofanywa na watuhumiwa ni vibaya na ambavyo kamwe haviwezi kuvumiiwa na jamii katika nchi.
Hivyo ametoa rai kwa wananchi kuacha kufanya uhalifu kwa kutumia mitandao kwani sheria yake iliyopitishwa na bunge hivi karibuni haitamwacha mtu akiwa salama.
Hata hivyo kamanda huyo ameomba polisi wapewe kifaa kama cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru na kukamilisha mwenendo wa kesi mapema.
Amesema, kwa sasa uhalifu kwa njia ya mitandao unakuwa kwa kasi duniani kote na kwamba, mtu anaweza kutenda makosa mengi yanayosumbua jamii ikiwemo wizi mkubwa na mdogo wa fedha kwenye benki, makosa ya udhalilishaji, lugha za matusi na mengine mengi.
Amesema kuwa, kupatikana na kifaa hicho kutasaidia ushahidi kuwa madhubuti na sio rahisi kumwondoa mtu katika hatia.
Pia amewataka wananchi wote hususan vijana kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao badala ya kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii
Safari ya kuelekea
kizimbani ikiwa imeiva.
Zuberi Thabit
mtuhumiwa wa ubakaji.
Idd Adamu mtuhumiwa
wa kurekodi video za ubakaji.
No comments:
Post a Comment