Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasaliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa (katikati) akimsikiliza
Mkuu wa Kivuko cha MV Kilambo kinachomilikiwa na TEMESA Jaston Mbawala wakati
wa ziara ya kikazi aliyoifanya mkoani Mtwara. Kulia kwa Waziri ni Mhandisi
Samwel Chibwana wa TEMESA Mtwara.
Meneja wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mtwara Mhandisi Saidi Mongomongo akimuelezea jambo
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa
alipotembelea kivuko cha MV Kilambo kilichopo mkoani Mtwara kinachotoa huduma mto
Ruvuma mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa akikagua injini ya kivuko
cha MV Kilambo kinachotoa huduma mto Ruvuma kati ya Kilambo, Tanzania na
Namoto, Msumbiji.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa ametembelea na kukagua kivuko
cha MV Kilambo kilichopo Mkoani Mtwara mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Kivuko
hicho kinavusha magari, abiria na mizigo kati ya Kilambo upande wa Tanzania na
Namoto Msumbiji.
Akiwa katika ziara hiyo
Profesa Mbarawa aliambatana na viongozi mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mkoani hapa. Profesa Mbarawa alikaribishwa na Mkuu wa Kivuko hicho Jaston
Mbawala, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wa Mkoa wa Mtwara
Mhandisi Saidi Mongomongo, Mhandisi
Msaidizi wa Kivuko Samwel Chibwana pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya
Ukodishaji Mitambo na Huduma za Vivuko Mhandisi Japhet Y. Maselle.
Akiwa kivukoni hapo,
Profesa Mbarawa alipata wasaa wa kusikiliza baadhi ya changamoto zinazokikumba kivuko hicho ambapo Mhandisi
Saidi Mongomongo alitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu wa maji nyakati za
kiangazi, ubovu wa maegesho ambayo husababisha magari makubwa kunasa wakati
yanatoka au kuingia ndani ya kivuko pamoja na kukosekana kwa boti ndogo za
uokoaji ambazo zingesaidia wakati wa dharura.
Baadae Profesa Mbarawa
alipata fursa ya kuongea na watumishi walio chini ya Wizara yake katika kikao
kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa mkoa huku akiwataka watumishi kuendelea kushirikiana na serikali, kufanya kazi
kwa kasi na uadilifu kwa kuzingatia weledi. Pia aliwataka watumishi kujenga
tabia ya kujitoa kwa ajili ya nchi yao.
Profesa Mbarawa alikuwa
kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kwa nia ya kutembelea na
kukagua utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake.
No comments:
Post a Comment