Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye amesema kuwa wasanii na watu wenye
majina makubwa ndio wanaoonekana zaidi katika athari za madawa ya kulevya
ingawa wapo wengi katika jamii wanayotumia madawa hayo.
Nape Nnauye ameyasema
hayo leo katika ukumbi wa Bunge, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa majibu kwa
waandishi wa habari waliotaka kujua namna ambavyo wizara yake imelipokea sakata
la kukamatwa kwa wasanii ambao wanatuhumiwa kutumia madawa ya kulevya.
“Kama wizara
inayosughulikia suala la wasanii tunaunga mkono juhudi zozote za kupambana na
jambo hili kwa sababu mwisho wa siku sehemu ya wadau wetu wanaathirika, hivyo
basi juhudi za kupambana nalo zinaokoa wadau wetu,” alifafanua Nape Nnauye.
Aliendelea kwa kusema
kuwa kama wizara inayosimamia wasanii wamekuwa wakijadili na kuzungumza juu ya
athari hizo za madawa ya kulevya kwa wasanii, aidha wapo wasanii ambao Serikali
imewasaidiwa kupata matibabu kutokana na athari za madawa hayo, akiwemo
mwanamuziki Rehema Chalamila anayefahamika kama Ray C.
Aidha amesema kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama wa Mkoa huo hivyo hawajibiki kuuliza Wizara hiyo anapotaka kuchukua
hatua zozote kwa wasanii waliopo ndani ya mkoa anaosimamia, lakini anapohitaji
anaweza kuiuliza wizara hiyo.
Nape Nnauye amesema
kuwa ni kazi kubwa sana kwa mtu kutengeneza jina (brand) lakini ni
rahisi sana kubomoa, hivyo basi ni vyema busara ikatumika katika
kuwashughulikia waathirika, vile vile watu wasihukumiwe kwa tuhuma.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitangaza majina ya watu wanaotuhumiwa kuuza ama kutumia madawa ya kulevya wakiwemo wasanii, maaskari na wafanyabiashara na kuwataka kuripoti Polisi kwa ajili ya mahojiano.
No comments:
Post a Comment