Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia
alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka mpya wa Mahakama leo jijini
Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai ripoti ya kesi za
uchaguzi wa mwaka 2015 katika hafla ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Mahakama
leo jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa TANZANIA Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Mahakama
kukusanya Shilingi Trillioni 7.3 ambazo ni matokeo ya Serikali kushinda kesi
mbalimbali za ukwepaji kodi.
Rais Magufuli
ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria
na Mwaka mpya wa Mahakama iliyobeba kauli Mbiu isemayo Utoaji haki kwa wakati
kuwezesha ukuaji wa uchumi.
Alisema kuwa
Takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na baadhi ya kesi za pingamizi za kodi ambapo Serikali
imeshinda kesi hizo japo fedha hizo hazijakusanywa mpaka sasa.
“Kukwepa au kutolipa
kodi ni kosa kubwa sana, kila mtu anawajibu wa kulipa kodi nchini kwa maendeleo
ya nchi” nalifafanua Dkt Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli
alisema kuwa katika kuelekea ukuaji wa uchumi, Mahakama iwe sehemu ya chanzo
cha pato la taifa kwa kwa kuhakikisha wale wanaotakiwa kulipa fidia baada ya
kushindwa kesi wanafanya hivyo pamoja na kuwabana wakwepa kodi kwani kutimiza hilo
kutaleta mabadiliko katika uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine
Rais Magufuli alisema kuwa Maendeleo ya nchi hayaangalii chama chochote, hivyo
amevitaka vyombo vya utoaji haki kutoa haki kwa usawa.
Kwa upande wake Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma alisema kuwa Mahakama imeandaa
Mpango mkakati uliolenga kufanya maboresho ndani ya Mahakama.
Alisema kuwa mpango
mkakati huo umelenga masuala makuu matatu ikiwemo Utawala bora, uwajibikaji na
usimamizi wa rasilimali, upatikanaji wa haki na kwa wakati, uimarishaji wa
amani kwa wananchi na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za mahakama.
Aidha Kaimu Jaji Mkuu
alisema kuwa Mahakama imefanikiwa kusikiliza mashauri ya kesi za uchaguzi kwa
asilimia 100.
“kati ya mashauri ya
kesi 249 ikiwemo 53 za ubunge na 196 za madiwani ya waliopinga uchaguzi kati ya
kesi hizo, kesi 52 za ubunge zilikamilishwa na kesi zote za madiwani
zilikamilishwa” alifafanua Kaimu Jaji Mkuu.
Naye Mwanasheria Mkuu
wa Serikali George Masaju amesema kuwa Katiba imeanisha bayana Kanuni ambazo
zinapaswa kuzingatiwa na Mahakama wakati ikitekeleza mamlaka yake ya utoaji
haki.
“utoaji haki mapema
ipasavyo ni moja ya Kanuni ambazo Mahakama inapaswa kuzingatia katika
utekelezaji wa majukumu yake kama inavyoelekezwa katika Katiba” alifafanua
Mwanasheria Mkuu.
Alisema kuwa Serikali
imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara katika nchi ya
Tanzania hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Siku ya Sheria nchini
ilioanzishwa mwaka 1996 ikiwa ni siku muhimu ya kuombea Majaji na Mahakimu ili
kuweza kusikiliza kesi.
No comments:
Post a Comment