Kampuni ya ORICA ambayo inafanya kazi za kulipua miamba ya dhahabu kwenye mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) na Buzwagi Imetoa vifaa tiba kwenye kituo cha afya cha Nyakumbu kilichopo kwenye kata hiyo wilaya na Mkoa wa Geita vyenye thamani ya shilingi Milion mbili(2000,000)
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ,Msimamizi msaidizi wa kituo cha Orica mwandisi Pascal Malugu,amesema kuwa walifikiria kuwa sio vyema kwenye jamii ambayo wanafanyia kazi kutokutoa mchango wowote ambao utasaidia jamii hivyo wakaguswa na kuamua kutoa vifaa tiba ambavyo vitasaidia kutoa huduma za kiafya huku akitoa wito kwa makapuni mengine kujitolea misaada mbali mbali.
“Leo hii si mara ya kwanza katika jamii kutoa misaada kwani tulishawahi kutoa kifaa kingine cha Eqbet kwenye hospitali ya Geita na sisi tuliona sio vyema kutotoa misaada ambayo itasaidia jamii inayotuzunguka lakini niombe Mashirika na Makapuni mengine kuguswa na kutoa misaada kwani hii ndio dini safi kuwasaidia ambao ni wagonjwa”Alisema Malugu.
Hata hivyo kwa upande wake msimamizi mkuu wa kampuni hiyo,Yahaya Ruyaga ameelezea kuwa wanaamini kuwa msaada ambao wameutoa utapunguza adha iliyokuwepo kwenye kituo hicho na kwamba ni mwanzo tu kwani wanajipanga kuendelea kutoa mchango zaidi kwenye maeneo yaliyopo ndani ya Mkoa wa Geita.
“Sisi kama saiti ya Geita tulikaa wafanyakazi na kuweza kufikiria kwamba je sisi kama sisi tunaweza kufanya kitu gani kwenye jamii ili walau na sisi tuweze kuleta faida kwenye jamii inayotuzunguka ndipo tulipoamua kuunda tume ya kufuatilia vituo vyetu vya afya vilivyopo kwenye halmashauri ya mji mwisho wa siku tukajua kituo cha Nyakumbu kina uhitaji mkubwa ndipo tulipoamua kutoa msaada huu wa vifaa tiba”Alisema Ruyaga.
Aidha mganga mfawidhi wa kituo hicho,Abdallah Amiry Kiroboto amesema kuwa vifaa walivyopatiwa vitawasaidia kurahisisha kazi na kwamba kwa sasa wataweza kupima magonjwa ya kisukari kutokana na kupatiwa kifaa hicho huku akiomba msaada kwa wadau wengine kufika katika kituo hicho na kuwasaidia kwani wana upungufu mkubwa wa vifaa vingi vya kufanyia kazi.
Baadhi ya wananchi ambao walikuwepo kwenye makabidhiano hayo wameishukuru kampuni hiyo kwa moyo wa kujitolea huku wakiomba makampuni ambayo yamo ndani ya mgodi wa GGM kuiga mfano wa kampuni hiyo.
No comments:
Post a Comment