Washiriki watatu wa
Tamasha la Majimaji Selebuka lililofanyika mkoani Ruvuma wanatarajia kushiriki
mashindano ya Mbio za Baiskeli nchini Afrika Kusini Februari 19, 2017.
Hayo yamebainishwa leo
na Muandaaji Mkuu wa Majimaji Selebuka Reinafrida Rwezaura wakati wa
makabidhiano ya tiketi za ndege za kwenda Afrika Kusini kwa washindi hao
yaliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dar es Salaam.
“Kikubwa
kilichotukutanisha hapa leo ni kuwaaga washindi wa Mbio za Baiskeli katika
tamasha la Majimaji Selebuka 2016, zilizofanyika tarehe 04 Juni 2016 kutoka
Mbinga hadi Songea umbali wa kilomita 100, ambao wanatakiwa kwenda kushiriki
mashindano ya Mbio za Baiskeli Jijini, Johanesburg, Afrika Kusini,” alifafanua
Rwezaura.
Rwezaura aliwataja washindi
hao wanaotegemea kwenda Afrika Kusini kuwa ni Salum Miraji ambaye alikuwa
mshindi wa kwanza , Allen Nyanginywa ambaye alikuwa mshindi wa pili
na Ipyana Mbogela ambaye alikuwa mshindi wa tatu.
Kwa upande wake,
mshiriki wa mashindano hayo Allen Nyanginywa ameishukuru Taasisi ya Songea
Mississippi (SO-MI) kwa kuandaa mashindano hayo pamoja na kutimiza ahadi ya
kuwasafirisha washindi wa kwanza hadi wa tatu kwenda nchini Afrika
Kusini.
Aliendelea kwa kusema
kuwa watahakikisha wanachukua ushindi nchini Afrika Kusini kwani huko wanaenda
kufanya kazi na wamefanya mashindano hayo ya Baiskeli imekuwa ni kazi yao.
Majimaji
Selebuka ni tamasha linalofanyika kila mwaka mjini Songea, mkoani Ruvuma ambalo
huandaliwa na Taasisi ya Songea Mississippi (SO-Mi) ambapo kwa mwaka
huu 2017 tamasha hilo linatarajia kufanyika kunzia Julai 23 hadi 30, 2017.
No comments:
Post a Comment