Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa msimamo wake juu ya Shirika
la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutopandisha gharama za umeme kwa wateja
wake upo palepale.
Prof. Muhongo
ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja
zilizowasilishwa na wabunge juu ya zuio la upandishaji bei ya umeme
kwa shirika hilo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya shughuli za Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini katika kipindi cha mwaka 2016/2017.
“Haiwezekani
wakapandisha bei ya umeme wakati kuna watu ndani ya Shirika wanamiliki hadi
hoteli nne, wakijaza lita 20 za mafuta katika magari wanaandika lita
50 na kila mwisho wa mwaka wanagawana milioni 50 kama ‘bonus’,” alifafanua
Prof. Muhongo.
Ameendelea kwa kusema
kuwa Shirika hilo linadaiwa kiasi cha shilingi Bil. 820, katika deni hilo kiasi
cha shilingi Bil.320 bado hazijachambuliwa. Hivyo shirika hilo haliwezi
kujiamulia kupandisha gharama ya umeme wakati huo huo wakiwa bado hawajachambua
baadhi ya madeni yao.
Aidha Prof. Muhongo
amesema kuwa, Shirika hilo linahitaji kiasi cha Dola Bil. 12 kwa ajili ya uwekezaji
ili ifikapo mwaka 2020 kiasi cha Mg 5000 za umeme ziweze kuzalishwa.
Hata hivyo, Prof.
Muhongo amesema amekwisha anza kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia ili kuona
kama wataweza kufadhili kiasi hicho cha fedha ili kiweze kuwekezwa katika
Shirika hilo.
Aliendelea kwa kusema
kuwa Shirika hilo linahitaji mabadiliko ya hali ya juu ili kulifanya kuwa la
kisasa na kuendana na dhima ya nchi ya uchumi wa viwanda ambao kwa
asilimia kubwa unahitaji nishati hiyo ya umeme.
No comments:
Post a Comment