Wafanyabiashara wa
Pombe za Kienyeji wanatakiwa kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo ambayo
hutolewa na Halmashauri.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo ameyasema hayo, Mjini
Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Najma Giga juu ya
Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la ulevi wa kupita kiasi kwa pombe
za kienyeji pamoja na sheria ya vileo ya mwaka 1969 kuwa ya zamani hivyo
kutokidhi mabadiliko ya hali halisi ya vileo.
“Pombe za kienyeji
zimeanishwa katika kifungu cha 2 cha tafsiri katika Sheria ya Vileo, Sura ya 77
ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, wafanyabiashara wote wanatakiwa kuwa na
leseni ambayo inatolewa na Halmashauri,” alifafanua Jafo.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, biashara hiyo hairuhusiwi kufanyika katika muda wa kazi. Muda
unaoruhusiwa kisheria ni kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku kwa siku
za Jumattu hadi Ijumaa na kuanzia saa 05:00 asubuhi hadi saa 06:00 usiku kwa
siku za Jumamosi, Jumapili na Sikukuu.
Vile vile amesema
kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi ni tabia ya mtu ambayo inawezekana kabisa
haitokani na mapungufu ya Sheria.
Hata hivyo Wakuu wa
Mikoa na Wilaya wameagizwa kusimamia taratibu za uendeshaji wa biashara za
vileo na kuchukua hatua kwa watumiaji na wafanyabiashara wanaobainika kukiuka
Sheria hiyo.
Aidha amesema kuwa,
endapo ipo haja ya kuifanyia marekebisho Sheria ya vileo, Serikali itakuwa
tayari kupokea mapendekezo kwa eneo ambalo litaonekana kuwa na mapungufu ili
kufanyiwa marekebisho kupitia Bunge.
Jafo ametoa wito kwa
Watanzania wote kutumia muda wao kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo
kwa ustawi wa Taifa zima. Aidha Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wanywaji
pombe wasiozingatia utaratibu pamoja na wazururaji wakati wa kazi.
No comments:
Post a Comment