Mtu yeyote atakaye
ruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la
mchezo wa kubahatisha (kamari) anahesabiwa kufanya kosa.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Asha Abdullah Juma juu ya kuongezeka kwa
maduka ya kucheza Kamari yanayojulikana kama Jack Pot katika miji mingi hapa
nchini hivyo kusababisha uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana.
“Michezo yote ya
kubahatisha ikiwemo kamari (slots machines) inaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya
Bodi ya Michezo ya kubahatisha namba 4 ya mwaka 2003, sura 41 pamoja na Kanuni
zake,” alifafanua Dkt. Kijaji.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, kwa mujibu wa sheria hiyo hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha
biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo
ya kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka nyingine za
biashara.
Vile vile sheria hiyo
inakataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au
kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
Aidha mtu yoyote
ambaye atamruhusu mtoto chini ya miaka 18, kushiriki, kuingia au kukaa karibu
na eneo la mchezo wa kubahatisha anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa
faini ya shilingi 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa
pamoja.
Dkt. Kijaji amesema
kuwa ikiwa kosa hilo litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi
inamamlaka ya kumfutia leseni.
Hivyo basi, wajibu wa
Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya
kubahatisha.
Pia, Dkt. Kijaji
ametoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia vijana wao kucheza michezo ya
kubahatisha pale wanapoona kuwa uchezaji wao unakuwa na matokeo hasi.
Hata hivyo amesema
kuwa, michezo hiyo inaendeshwa kwa mujibu na sheria kama shughuli nyingine.
Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, wanaoendesha michezo hiyo wanazingatia
sheria na kanuni zilizowekwa pamoja na wazazi, walezi na jamii kuhakikisha
vijana wanazingatiia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania
wanapokuwa wanajishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment