Bunge la Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2016 [The written laws
miscellaneous Amendments (No. 4) Bill, 2016].
Akiwasilishwa muswada
huo Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa muswada
huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Sita ambapo lengo la
marekebisho yanayopendekezwa ni kurahisisha utekelezaji wa Sheria hizo kwa
kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia masharti ya sheria hizo.
Masaju alizitaja
sheria zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia muswada huo kuwa ni
Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,
Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Sukari na
Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori.
“Ibara ya 21 ya
muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 30 cha Sheria ambacho
kinaweka masharti kuhusu Waziri mwenye dhamana ya fedha kukasimu madaraka yake
chini ya Sheria hiyo. Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa Waziri anaweza
kukasimu mamlaka yake ya kujadili mkopo (negotiating loan), kuingia makubaliano
ya kukopa mkopo na kutoa dhamana,” alifafanua Masaju.
Aliendelea kwa kusema
kuwa muswada unapendekeza kuwa Waziri awe na uwezo wa kukasimu pia mamlaka ya
kujadili au kuingia makubaliano ya misaada kwa mamlaka au mtu mwingine. Lengo
la marekebisho hayo ni kurahisisha taratibu za upokeaji misaada kwa kuwa sheria
hiyo ilikuwa kimya kuhusu suala hilo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa
alipokuwa akitoa maoni na ushauri wa kamati hiyo alisema kuwa, kamati hiyo
inaunga mkono marekebisho ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu kwa sababu itatoa
nafasi kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini kupata nafasi ya kusoma katika
Vyuo vya Elimu ya Juu.
Aidha ameeleza kuwa,
kamati inakubaliana na mtazamo wa Serikali kwamba utoaji wa Mikopo ya Elimu ya
Juu kwa ajili ya ngazi ya Diploma utazingatia vipaumbele vya Taifa kulingana na
wakati husika.
Nae, Mbunge wa
Karagwe, Innocent Bashungwa amesema kuwa muswada huo umelenga
kusaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu.
Vile vile muswada huo
unapendekeza marekebisho katika sheria ya Wanyamapori kuwa, katika hatua yoyote
ya kesi ya Mahakama inaweza kwa kuamua yenyewe au kwa maombi ya
upande wa mashtaka kutoa amri kuwa mnyama, nyara ya Serikali, silaha, gari au
kitu chochote kilichotolewa kama ushahidi ambacho kinaweza kuharibika au
kupoteza thamani kiuzwe au kiharibiwe na Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia muswada huo
unapendekeza kuongezwa kifungu kipya kitakachoweka masharti kuhusu bei elekezi
ya miwa, sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na miwa.
Mwenyekiti,
Mhe. Najma Giga alitangaza rasmi kupitishwa kwa muswada huo na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi za ndio. Aidha muswada huo
unasubiri kibali cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili uanze kutumika kama
sheria.
No comments:
Post a Comment