Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa
kwa atakayepokea rushwa kutoka kwa wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa Madawa
ya Kulevya.
Ameyasema hayo leo
jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha Baraza la Taifa
la kudhibiti dawa za kulevya nchini.
“Sheria ya udhibiti wa
madawa ya kulevya itumike vizuri, Serikali na Baraza halitahitaji mtu yeyote
mwenye mamlaka kupokea rushwa ikigundulika hatua kali zitachukuliwa” alifafanua
Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu
alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha
mapambano dhidi ya udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo yamekuwa
yakifanywa na Serikali za Awamu zilizotangulia.
Aidha, Waziri Mkuu
alisema kuwa mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ni vita inayotakiwa kupigana
kwa nguvu kubwa kwani madhara ya dawa hizo ni kubwa kwa jamii hususani vijana
ambao ni nguvu kazi ya taifa.
“Tunahitaji ushirikiano
wa karibu wa pande zote mbili za Muungano kwani tatizo hili limeathiri pande
zote na ukanda wa bahari unatumika sana kama njia ya kuingiza dawa hizo”
“Wakuu wa Mikoa mna
kazi kubwa katika vita hii, mkiwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama mpo
kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo Waziri Mkuu
alibainisha kuwa, wajibu wa Baraza ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Udhibiti
wa Dawa za Kulevya nchini, ambapo jukumu hilo ni kubwa na wajumbe wa Baraza
hilo wanatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu na umahiri mkubwa.
Baraza la Taifa la
kudhibiti Dawa za Kulevya limeanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 ambapo Waziri
Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wajumbe wengine wakiwemo Waziri
anayeshughulikia Mambo ya Sheria, Waziri anayeshughulikia Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Wengine
ni Waziri anayeshughulikia Afya, waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii,
Waziri anayeshughulikia Mambo ya Nchi za Nje, Waziri anayeshughulikia Fedha,
Waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Waziri anayeshughulikia Elimu,
Waziri anayeshughulikia Kilimo, Waziri anayeshughulikia Uchukuzi na Waziri
anayeshughulikia Ulinzi.
No comments:
Post a Comment