Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Mosses Nnauye.
Nchi za Afrika
Mashariki zimekubaliana kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili kuwa Tanzania
ambayo yatakuwepo Zanzibar.
Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma
alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya jitihada mbalimbali ambazo Tanzania
inazichukua katika kukuza Lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Kimataifa.
Nape amesema kuwa
maamuzi hayo ya kuifanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili
yametokana na Tanzania kuzalisha walimu wengi wa Kiswahili ambao wanatumika
katika ngazi mbalimbali za elimu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Anastazia Wambura amesema kuwa Wizara hiyo kwa sasa
inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa mawakala
wa kulinda Lugha ya Kiswahili ambapo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)
kwa kushirikiana na wadau wa Kiswahili limeendelea kuendesha semina, warsha,
makongamano na kutoa elimu inayohusu matumizi fasaha ya Lugha ya Kiswahili.
Aidha, aliendelea kwa
kusema kuwa Waandishi wa Habari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Lugha hiyo
inaendelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya Lugha
hiyo katika majukumu yao ya kila siku.
“Kutumia zana kama
vile Kamusi na vitabu vya miongozo ya uandishi pamoja na kuhudhuria makongamano
ya Kitaifa na ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili inasaidia kuongeza ujuzi na
uweledi wa Lugha ya Kiswahili, kujua istilahi za kisayansi na
kiteknolojia na hivyo kuandika na kutangaza kazi bora na zenye maudhui lengwa
kwa jamii na kuepuka upotoshaji wa maneno ya Kiswahili usio wa lazima,”
alifafanua Anastazia Wambura.
Hata hivyo Wizara hiyo iko katika maandalizi ya Sera ya Lugha ambayo itabainisha majukumu ya Vyombo vya Habari katika matumizi na uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.
No comments:
Post a Comment