Ada za uhakiki wa
filamu hapa nchini zipo kwa mujibu wa sheria na kanuni, ambapo gharama hizo
hulipwa kwa nakala mama na baada ya hapo mtayarishaji huzalisha nakala kwa
idadi anayohitaji.
Naibu Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Anastazia Wambura ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini
Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi juu ya
Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama za ukaguzi ambapo kwa
hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja kwa dakika.
“Nchi yetu hutoza ada
ambazo ni rafiki ukilinganisha na nchi nyingine, kwa mfano, Nigeria ambayo ni
nchi iliyopiga hatua kubwa kwa upande wa filamu, hutoza filamu yenye urefu wa
dakika 60 (filamu ya lugha asili) Naira 30,000 sawa na zaidi ya dola 150 ambayo
ni sawa na Sh. 337,950 za Kitanzania na Kenya, ni sawa na Sh. 190,000,”
alifafanua Anastazia Wambura.
Aliendelea kwa kusema
kuwa Tanzania hutoza filamu za Kitanzania zenye urefu wa dakika 60 kwa Sh.
60,000 (sawa na Sh. 1,000 kwa dakika) ambapo gharama hizo ni sawa na asilimia
18 ya gharama za Nigeria na asilimia 32 ya Kenya.
Hivyo basi Tanzania
imekuwa ikitoza ada hiyo ya uhakiki wa filamu kwa gharama nafuu na rafiki
ukilinganisha na nchi nyingine Afrika.
Akijibu swali la namna
gani Bodi hiyo imejipanga kuhakikisha huduma zao zinatambulika nchi nzima
tofauti na sasa ambapo wasanii wachache ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu ya
Bodi hiyo, Wambura amesema kwamba Bodi hiyo imeendelea kujitangaza kwa wadau
kupitia shughuli mbalimbali za kitaifa na Kimataifa kama vile kushiriki katika
maonesho ya Sabasaba.
Vile vile bodi hiyo
imekuwa ikishiriki katika wiki ya Vijana na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festivals (JAMAFEST). Pia
hutumia vyombo mbalimbali vya habari kama vile TBC1, E-FM, Clouds media pamoja
na magazeti mbalimbali kueleza watanzania kazi zinazofanywa na Bodi hiyo.
Aidha Bodi hiyo
imekuwa ikifanya warsha za kuwajengea wadau wake weledi katika masuala ya
filamu sehemu mbalimbali ikiwemo mikoani na wilayani ikiwa
ni moja ya maeneo ya kujitangaza.
No comments:
Post a Comment