Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde
Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana umetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi 1,867,896,520 kwa vikundi vya
vijana 309 katika Halmashauri 94.
Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde ameyasema
hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalum Zainab Katimba alipotaka kujua idadi ya vijana walionufaika kupitia
mfuko huo na namna ambavyo mikopo hiyo imebadilisha maisha yao.
“Lengo la kuanzishwa
kwa mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini (Tanzania
Bara) kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au
kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali,” alifafanua Mavunde.
Aliendelea kwa kusema
kuwa fedha za mikopo zitokanazo na Mfuko huo umekuwa msingi mzuri katika
kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine na hata kukuza vipato
vyao.
Mavunde alitaja
shughuli ambazo vijana hao wamekuwa wakishiriki mara wanapopata mikopo hiyo
kuwa ni uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, kilimo, ufugaji pamoja usindikaji
wa mazao.
Aidha amesema kuwa
shughuli hizo zimewafanya vijana kuachana na utegemezi na badala yake kutumia
muda wao mwingi katika kuzalisha na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Nchi.
Vile vile amesema
kwamba, vipo vikundi ambavyo kupitia mfuko huo vimekuwa kielelezo cha dhati
katika kubadili mtizamo wa vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi
kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao.
Alivitaja vikundi
hivyo kuwa ni kikundi cha Thyroid Group kutokana Halmashauri ya Chunya ambacho
kinasambaza Taa za Solar Vijijini, kikundi cha Miranaco Group ambacho
kinamiliki duka kubwa la dawa za Binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, kikundi
cha Maswa Family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk
kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.
Aidha, ili kuboresha
mfuko huo Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara
kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za kiutendaji
zinazojitokeza.
Hata hivyo, katika
mwaka huu wa fedha Serikali inapitia upya mwongozo wa utoaji fedha kupitia
mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana ambao ulioanzishwa mwaka 2013
ili kuwawezesha vijana wengi kuanzisha viwandaa vidogo vidogo katika
kuendana na Sera ya Nchi ya kwenda kwenye Uchumi wa Viwanda.
No comments:
Post a Comment