Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa amezitaka Taasisi zote za Umma ambazo zinadaiwa na Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL) kuhakikisha zinalipa madeni yao kabla ya Juni 30, 2017.
Waziri Mkuu ametoa rai
hiyo leo, Mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge wakati wa uzinduzi wa huduma ya
4G LTE za kampuni hiyo ya simu kwa Mkoa wa Dodoma.
“Kuhusu shilingi Bil.
11.5 ambazo TTCL inazidai Taasisi mbalimbali za Umma, Mheshimiwa Waziri wa
Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, kaa na wadaiwa sugu wote, thibitisheni madeni
husika kisha mkubaliane namna ya kulipa madeni hayo. Nijuavyo kila Wizara
inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za simu, sasa hayo malimbikizo yanatoka
wapi?” alisema Kassim Majaliwa.
Aidha amezitaka
Taasisi hizo zinazodaiwa na TTCL kuhakikisha zinakamilisha madeni yao kabla ya
kufikia Juni 30, 2017 ili kampuni hiyo iweze kufanya kazi ipasavyo na kuendana
na ushindani wa kibiashara uliopo.
Pia, ameitaka kampuni
hiyo kujifunza kutoka kwenye makampuni binafsi namna yanavyoendeshwa na kuiga
baadhi ya mbinu zao, hususan katika kupunguza gharama za uendeshaji.
Kassim Majaliwa
amesema kwamba, Serikali ina matarajio makubwa kutoka katika kampuni hiyo
kutokana na kuwa na imani kwamba kampuni hiyo ina maarifa ya kujifunza kutoka
kwa waliofanikiwa kwenye sekta hiyo.
Vile vile ameitaka
kampuni hiyo kujifunza kutoka katika mashirika ya Umma ya Simu kwenye nchi
nyingine ambayo yanajiendesha kwa faida, kwa kuiga mbinu ambazo wanazitumia na
kuziweka katika muktadha wa nchi ya Tanzania.
Waziri Mkuu
amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
pamoja na timu yake kwa hatua ambayo kampuni hiyo imefikia. Aidha amemtaka
Waziri huyo kufuatilia kwa karibu kampuni hiyo ili iweze kutoa ushindani wa
kutosha kibiashara, ijiendeshe kwa faida, itoe gawiwo stahiki kwa Serikali,
ilipe kodi na zaidi ya yote fedha za Umma zilizowekezwa ziweze kutumika vizuri.
No comments:
Post a Comment