Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene
amesema kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Simbachawene ameyasema
hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Jimbo la Chemba Juma Nkamia kuhusu Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa
wababe katika maeneo yao ya kazi.
“Wakuu wa Mikoa na
Wilaya wanasimamia maeneo yao kwa mujibu wa sheria na wana haki ya kuwachukulia
hatua watumishi ambao hawatekelezi majukumu waliyopewa,” alifafanua
Simbachawene.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, hata kama kuna Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni wababe katika maeneo yao
ya kazi hauwezi kusema kila Mkuu wa Mkoa au Wilaya aliyechukua hatua dhidi ya
mtumishi ambaye hawajibiki katika kazi yake ni mbabe au muonevu.
Aidha, Simbachawene
amesema kuwa ni wakati sasa wa watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao na
kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Kwani hakuna kiongozi ambaye ataweza kumchulia
hatua mtumishi ambaye anawajibika na kazi zake kama alivyopangiwa.
Vile vile amesema
kuwa, wakuu hao wa Mikoa na Wilaya wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika maeneo
wanayoyasimamia, kutokana na watumishi wengi wa Serikali walikuwa wamejisahau
kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kimazoea.
No comments:
Post a Comment