Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji
Serikali haina mamlaka
ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa
mikopo.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Machano Othman Said juu ya
lini Serikali itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia asilimia
10 – 12 badala ya sasa ambayo ni asilimia 17 – 20.
“Mabadiliko ya Sekta
ya Fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja
kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria,
hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na
gharama nyingine za huduma za kibenki,” alifafanua Dkt. Ashatu Kijaji.
Aliendelea kwa kusema
kuwa viwango vya riba za mikopo na riba za amana pamoja na riba za mikopo kati
ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha,
gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na hatari
ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Aidha Dkt. Ashatu
Kijaji amesema kuwa kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba
katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya
kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki
Kuu imeelekeza.
Vile vile amesema kuwa
kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na
mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo, ambapo kwa sehemu kubwa
gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji wa fedha
pamoja na gharama za uendeshaji.
Pia amesema kuwa, ni
muhimu kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa juu, ndivyo riba za
amana zinapokuwa juu pia, ambapo wastani wa riba za kukopa kwa mwaka mmoja
mwezi Juni, 2016 ulikuwa asilimia 13.67 wakati wastani wa riba za amana za
mwaka mmoja ulikuwa asilimia 11.52 ikiwa ni tofauti ya asilimia 2.25.
No comments:
Post a Comment