Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangala
Serikali inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa
pombe za bei rahisi maarufu kama “Viroba” Nchini, ndani ya miezi mitatu ijayo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Hamisi Kigwangala ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma
alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi
hicho kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za
kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi pamoja na Huduma na Maendeleo ya
Jamii kwa mwaka 2016/17.
Dkt. Kigwangalla amesema kuwa baada ya miezi mitatu kilevi hicho
kitapigwa marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya
yote ya uingizaji wa kilevi hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa na vijana wengi,
hivyo kuharibu nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko
amesema kwamba pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio
tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.
“Katika kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni
kwangu na tumezika vijana wanne ambao wamefariki kutokana na matumizi ya
viroba. Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari
za pombe hiyo ili tuweze kujadili na kuona namna gani ya kuliokoa
Taifa hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.
Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa
kati ya matumizi ya pombe hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia
ongezeko la vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha amesema kuwa hali hiyo inaathiri ufanisi
wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Hivyo Kamati imeishauri Serikali kufungia kabisa uzalishaji na uuzwaji wa pombe
hizo za viroba ili kulinusuru Taifa.
No comments:
Post a Comment