Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani
Ugunduzi wa gesi
asilia nchini umepelekea kushuka kwa gharama za umeme kwa asilimia 33.26 kwa
mwaka 2014 hadi 2016.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo leo Bungeni, Mjiji Dodoma
alipokuwa akijibu swali la Mbunge viti Maalum Maida Hamad Abdallah kuhusu faida
zilizopatikana tangu kugundulika kwa gesi asilia.
“Faida kubwa
iliyopatikana kutokana na ugunduzi na matumizi ya gesi asilia nchini ni
uzalishaji wa umeme wa bei nafuu kwa kutumia Gesi Asilia ikilinganishwa na
mafuta. Uzalishaji umeme kwa kutumia Gesi Asilia umeongezeka kutoka uniti
2,714.25 milioni kwa mwaka 2014 hadi uniti 4,196.4 milioni mwaka 2016 sawa na
ongezeko la asilimia 54.61,” alifafanua Dkt. Kalemani.
Aliendelea kwa kusema
kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa Gesi Asilia umepelekea kushuka kwa
bei ya umeme kutoka wastani wa shilingi 188.56 kwa uniti mwaka 2014 hadi
wastani wa shilingi 125.85 kwa uniti mwaka 2016.
Akitolea ufafanuzi
zaidi juu ya faida zinazopatikana kutokana na matumizi ya Gesi Asilia, Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa maeneo ya Mikocheni,
Jijini Dar es Salaam zikiwemo nyumba za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) wanatumia Gesi Asilia ambapo gharama wanayoitumia kwa mwezi
haizidi shilingi elfu 25,000, na wanatumia kwa kupikia aina zote za vyakula
hata vile vinavyotumia muda mrefu kuiva kama vile maharage na makongoro.
Aliendelea kwa kusema
kuwa, mpaka sasa jumla ya viwanda 37 vinatumia nishati inayotokana na Gesi
Asilia, ambayo gharama yake ni nafuu ukilinganisha na gharama ya nishati
nyingine.
Aidha, amesema kuwa
Wizara yake imepata ufadhili wa Dola Mil. 150 kutoka Afrikan Development Bank
kwa ajili ya kusambaza gesi katika mikoa Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.
Prof. Muhongo amesema
kuwa usambazaji huo utakapoanza na kufika maeneo ya Kinyerezi, Jijini Dar
es Salaam yatafungwa mabomba mengine kwa ajili ya kupeleka gesi katika mikoa
mingine kama vile Morogoro, Mbeya na Iringa.
Aidha amesema gesi
ambazo zinatumika kwa sasa ni gesi salama ambazo hazilipuki ukilinganisha na
gesi za miaka ya nyuma.
Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC) lilianza utafiti wa masuala ya mafuta na Gesi Asilia
nchini mwaka 1950, ikihusisha utafiti katika maeneo ya bahari ya kina kirefu,
maziwa na nchi kavu. Gesi Asilia iliyogundulika katika maeneo ya bahari ya kina
kirefu ni futi za ujazo trilioni 47.08 na katika nchi kavu ni futi za ujazo
trilioni 10.17 hivyo kuwa na jumla ya futi za ujazo trilioni 57.25 za Gesi
Asilia inayojulika kama “sweet gas” yaani gesi yenye kiwango kidogo sana cha
salfa (sulphur).
No comments:
Post a Comment