Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa REA wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi.
Mkoa wa Geita unatarajia kunufaika na mradi kabambe wa usambazaji umeme
vijijini REA awamu ya Tatu kwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi
kutokana na vitongoji 220, vijiji 372 na Kata 499 ambazo
zinatarajia kunuifaika na Nishati ya Umeme.
Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi REA meneja wa TANESCO
Mkoani Geita Joachim Ruweta amesema Mradi huo kwa mzunguko wa kwanza
utaunganisha wateja wapatao 12,944 na hivyo kukamilika kwa Mradi huo utafanya
umeme kuongezeka kwa Asilimia 51 kwa wateja waliopo sasa.
“Mategemeo yetu ni kwamba mzunguko wa pili ambao unatarajia kuanza mwaka
2019 na kumalizika mwaka 2020 na 2021 utafanya vijiji vyote vya Mkoa wa Geita
kupata umeme kwa asilimia mia moja” Alisema
Ruweta.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi amewataka
wananchi kutoa ushirikiano na kujua kuwa hakuna fidia ambazo watalipwa kutokana
na mradi huo.
“Wito kwa wananchi wa Mkoa wetu
wa Geita watoe ushirikiano Katika vijiji vyote ambako wataalamu wetu watapitia
wajue kuwa hakuna fidia kwasababu mradi huu utakuja kwaajili ya kutupatia
maendeleo na unapowasha umeme itasaidia kukua kwa uchumi wa eneo husika na Mkoa
wetu” Alisema Luhumbi.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa REA Gedion Kaunda alisema hadi sasa
hivi bado hawajaona tatizo lolote ambalo lipo kwenye mradi huo na kwamba
wanaamini watafanikisha kwenye maeneo yote ambayo mradio huo umepangwa
kufanyika.
Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza Mkoani Geita unatekelezwa
na mkandarasi aitwaye White city Guangdong JV ambaye ni ubia wa Kampuni ya
Kitanzania na Kampuni ya nje na unatarajia kugharimu zaidi ya Shilingi za
kitanzania Bilioni 61 na fedha za Kimarekani Dola milioni 7.8.
|
No comments:
Post a Comment