Friday 18 March 2016

WATU WAWILI WAFARIKI DUNIA NA WENGINE 13 KUJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI MBEYA.



Watu wawili wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Ndenjela linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam kuligonga kwa nyuma basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo ni daladala linalofanya safari zake kati ya Igawilo na stendi kuu jijini Mbeya katika eneo la Uyole, kwenye barabara kuu ya Tanzania - Zambia.



Ajali hiyo imetokea majira ya alfajiri wakati basi la kampuni ya Ndejela likitokea gereji kwenda katika kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya kwa ajili ya kuchukua abiria ili kuanza safari ya kwenda Dar es Salaam, lakini lilipofika eneo la Kilimo katika bonde la Uyole, ndipo basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo lilikuwa limesimama kituoni,likaingia ghafla barabarani na ndipo lilipogongwa na kwa nyuma na basi hilo la Ndenjela ambalo lilikuwa kwenye mwendo mkali na kusababisha daladala hilo kuacha njia na kugonga jiwe kubwa kando ya barabara.

Afisa muuguzi msaidizi wa zamu katika hospitali ya rufaa Mbeya,Abdul Kumwambe amethibitisha kuwepo kwa vifo vya watu wawili pamoja na majeruhi 13 ambao wanatokana na ajali hiyo.


Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi,Ahamed Msangi amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa basi la kampuni ya Ndenjela huku akidai kuwa uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.

No comments:

Post a Comment