KITAIFA


MGODI WA GEITA GOLD MINE(GGM) WALALAMIKIWA NA BAADHI YA WAKAZI WA MKOA WA GEITA.

Mgodi wa Geita Gold Mine(GGM)

Wakazi wa mitaa ya Nyamalembo ,Compound na Katoma mkoani Geita wameulalamikia mgodi wa Geita gold mine (GGM) kutokana na kuweka bikoni katika maeneo ya makazi yao zikionyesha kuwa eneo hilo ni mali ya mgodi huo hali ambayo imesababisha wananchi hao kushindwa kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Hayo yamebainishwa leo na wakazi wa maeneo hayo katika ziara ya naibu waziri wa nishati na madini alipotembelea maeneo hayo ili kujionea adha hiyo huku wakimuomba kulichukulia hatua za haraka  jambo hilo.

Kwa upande wake kaimu Afisa mahusiano wa mgodi huo Bw.Simon Shayo amesema kuwa kampuni hiyo haitambui madai hayo jambo ambalo limewashangaza wanachi wa maeneo hayo kutokana na kuzuiwa kufanya shughuli zao kwa muda mrefu.

Hata hivyo baada ya afisa huyo kukana kuwa kampuni haitambui zuio hilo naibu waziri wa nishati na madini Mh.Medadi Kalemani amewaagiza wananchi wamaeneo hayo kuendelea na shughuli zao huku akidai kuwalipa fidia wale waliokuwa wakidai kuzuiwa kufanya shughuli zao pindi mgodi utakapohitaji maeneo hayo.


Aidha ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kushirikiana na viongozi kushughulikia suala la maendeleo kwani kufanya hivyo itasaidia kuongeza chachu ya maendeleo mkoani hapa na taifa kwa ujumla.

WATOTO WANNE WA FAMILIA MOJA WENYE ULEMAVU WA VIUNGO MKOANI GEITA WANAHITAJI MSAADA.


                   
                      Watoto wa mzee Shikome Saliboko wenye ulemavu.

            Mtangazaji wa Stormfm(kati) Joel Maduka akiwa pamoja na watoto wenye ulemavu.

                      
                        Watoto wa mzee Shikome Saliboko wenye ulemavu.

Famila ya Shikome Saliboko yenye watoto wanne ambao wote ni walemavu wa viungo wanaomba msaada kwa wasamalia wema ambao wataguswa  kuwasaidia misaada mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu na mahitaji mengine.

Storm habari ilifika kijijini hapo na kuzungumza na kaka wa watoto hao Costantine Kizalia amesema kuwa tangu kufariki kwa baba yao mzazi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kimaisha moja wapo ni kukoswa mahitaji ya kila siku ikiwemo  mavazi,chakula na masomo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Saimon Shikome ambae ni mlemavu amewaomba wananchi wenye mapenzi mema pamoja  na serikali kuwapatia msaada wa kielimu kwani wanaamini elimu ndio msingi pekee ambao utawawezesha kupiga hatua za kimaisha.


Kwa upande wake mtendaji wa kijiji hicho Ugugwe Isalika,amesema kuwa mpaka sasa bado wanaendelea na jitihada  za kuhakikisha kuwa watoto hao wanapatiwa misaada lakini pia amewaomba wananchi kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia

SABABU KUU NNE ZA ANGUKO LA SHULE ZA VIPAJI KATIKA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE NCHINI.


              Dkt.Joyce Ndalichako, Waziri wa elimu,sayansi,teknolojia na mafunzo ya ufundi.

Anguko la shule za sekondari za Serikali zikiwamo za vipaji maalumu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, limedaiwa kusababishwa na walimu kukata tamaa, miundombinu duni na mazingira magumu ya kufundishia na kusomea.


Shule za vipaji maalumu, zinazochukua wanafunzi wanaofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba, hazimo kwenye orodha ya shule 50 bora, na kati yao ya kwanza inashika nafasi ya 53.

Orodha hiyo imetawaliwa na shule binafsi na za taasisi zisizo za serikali, hasa za kidini wakati za Serikali zinapambana kuanzia nafasi ya 53.

Kukata tamaa kwa walimu na mazingira magumu ya kufundishia ndiko kumeelezwa na wachambuzi mbalimbali kuwa ndiyo sababu kuu ya kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu kwa shule hizo.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alitaja shule 10 bora juzi kuwa ni Kaizirege ya Kagera, Alliance Girls (Mwanza), St Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam), na Marian Boys (Pwani).

Nyingine ni Alliance Rock Army (Mwanza), Fedha Girls (Dar es Salaam), Feza Boys (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Kaizirege kuongoza katika mitihani ya kitaifa huku Alliance Boy na Girls zikiwamo pia katika 10 bora kwa miaka mitatu mfululizo.

 Anguko la shule za Serikali 
Kuanguka kwa shule hizo kumedhihirika juzi mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne ambayo sehemu kubwa hazikufanya vizuri.

Dk Msonde alizitaja baadhi ya shule za sekondari za vipaji maalumu kuwa ni Ilboru ambayo imeshika nafasi ya 53, Kibaha (69), Kilakala (94), Mzumbe (71), Tabora Boys (124), Tabora Girls (128) na Msalato (148).

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa Utafiti na Sera wa Taasisi ya Hakielimu, Godfrey Boniventure alisema anguko hilo linaonyesha wazi kuwapo kwa tabaka kubwa kati ya walionacho na wasio nacho.

“Shule zote 10 za mwisho ni za Serikali ambazo wanasoma watoto wa maskini. Kibaya zaidi hata za vipaji maalumu zilizokuwa zikitegemewa zipo hoi. Hii ni hatari kwa Taifa,” alisema.

Alisema tabaka hilo litawafanya watoto wanaotoka kwenye familia zenye uwezo kupata nafasi za juu kwenye soko la ajira, huku maskini wakishindwa kuingia kwenye ushindani huo.

Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala alisema anguko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukata tamaa kwa walimu.

Alisema walimu hawana moyo wa kuendelea kufanya kazi hiyo na utafiti kwenye baadhi ya shule unaonyesha wengi wao wanaingia darasani kukamilisha ratiba na si kufundisha.

Profesa Mpangala alisema sababu iliyowafanya kufikia hatua hiyo ni Serikali kutowalipa stahiki zao kama mishahara, motisha, makato na mazingira magumu ya kufundishia.
Ilitokea kwangu. Niliamua kumhamisha mwanangu aliyekuwa akisoma shule ya vipaji maalumu kwa sababu walikuwa hawaingii darasani, sikuwalaumu hata kidogo, niliona wazi mazingira yao ya kazi ni magumu.”

Alisema sera ya elimu bure itachangia anguko kubwa zaidi kutokana na hali ya shule hizo kuendelea kuwa mbaya. Majengo ya shule za vipaji maalumu yamechoka, Serikali haipeleki pesa na wazazi hawachangii. Kitakachotokea hapo ni kufeli zaidi,” alisema.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema kukata tamaa kwa walimu kunachangia shule hizo kufanya vibaya.

Aliitaka Serikali kurejesha hadhi ya shule zake ili ziendelee kuwa kimbilio la wanyonge.
Kiwango cha  walimu katika ufundishaji  kimeshuka kwa kiwango kikubwa, Serikali isipotoa kipaumbele kwa kundi hili, itakuwa hatari zaidi,” alisema.

Ilboru wanena 
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Julius Shura alikiri kuwa hali ya shule hiyo ni taabani kutokana na kuchakaa kwa miundombinu.

Hata hivyo, tumejitahidi kutoa wanafunzi wawili bora ambao wametokana na jitihada zetu walimu licha ya kuwa mazingira ya kufundishia ni magumu. Tunaomba Serikali itupie jicho shule hizi ambazo zilikuwa taa kwa watoto wa Kitanzania wenye vipaji maalumu,”alisema.

Hali ni ngumu zaidi kwa watoto wenye ulemavu, hakuna mazingira rafiki hata kidogo. Piga picha bajeti ya Sh1,500 kwa mtoto anayesoma sayansi ni ndogo sana kwa siku, usitegemee kwamba atafanya maajabu,” alisema.

Siri ya shule binafsi kuongoza 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo Vya Serikali (Tamangsco), Benjamin Nkonya alisema siri ya shule zao kuongoza ni kuwekeza kwa walimu.


“Tunawasikiliza walimu, kuwapa heshima wanayostahili na kuhakikisha wanapatiwa kila wanachohitaji kama mikopo ya magari na nyumba, ukimjali mwalimu mengine yote yatakwenda vizuri,” aliongeza .


WACHIMBAJI MKOANI GEITA WAFUNGA BARABARA WAKIDAI MABAKI YA MAWE (MAGWANGALA).

Wachimbaji wadogo wa mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)
Tamko lililotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wachimbaji wadogo watapewa mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu magwangala kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) limesababisha wakazi wa Mtaa wa Nyakabale kufurika mgodini hapo kusubiri ahadi hiyo.
Vijana hao zaidi ya 800 walisema kuwa wamekusanyika kwa kuwa Serikali ilitangaza kutoa magwangala Februari 28.
Akizungumza na umati wa vijana hao Kaimu Ofisa Madini wa Mkoa wa Geita, Fabian Mshai aliwataka vijana hao kuwa watulivu na kutii sheria za nchi kipindi hiki ambacho tume iliyoundwa kufuatilia suala la magwangala, imepeleka maoni kwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kujua utaratibu utakaotumika.
Mshai alisema lazima taratibu zifuatwe ili kuepuka kuhatarisha uhai wa wananchi kwa kugombana wakati wakinyang’anyana mawe.
Alisema pia wanaweza kuharibu mazingira kwa kuwa kuna kemikali kali zinazotumika wakati wa uchanjuaji wa dhahabu.
Alisema kitendo kinachofanywa na wachimbaji wadogo walioamua kuanza kuingia katika maeneo ya mgodi na kuchukua mawe ni kukiuka sheria za madini na kuhatarisha maisha yao.
Diwani wa Mgusu, Pastory Ruhusa aliwataka wachimbaji wadogo kuwa watulivu na kuiomba Serikali kuharakisha taratibu za kutoa magwangala kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la wananchi kutokana na ahadi waliyopewa.
Alisema, juzi vijana hao walifunga barabara baada ya kuitwa wakimbizi na kusababisha wananchi kushindwa kusafiri kwenda nje ya kijiji na kusababisha usumbufu kwa wagonjwa na wananchi. 0.3k 0a

No comments:

Post a Comment