Friday 4 March 2016

MAGEUZI YA ARV ZA SINDANO KATIKA KUKABILI VIRUSI VYA UKIMWI DUNIANI.


Ni tiba inayoleta mapinduzi ya vita dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa sababu sindano moja itakuwa mbadala wa kumeza vidonge vya mwezi au zaidi.

Ni kweli kwamba kwa sasa hakuna dawa inayoweza kuponyesha Ukimwi, lakini kuna dawa za kupunguza makali na kutibu athari zinazotokana na maambukizi ya virusi vyake.
Kwa muda mrefu sasa, watu wenye maambukizi ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini na wale wanaougua maradhi nyemelezi, wamekuwa wakitumia vidonge kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa sasa matibabu ya Ukimwi kwa kutumia vidonge yanawalazimisha watumiaji wa dawa hizi kumeza aina tatu za dawa au zaidi kila siku.
Ingawa utaalamu wa kuunganisha dawa zaidi ya moja umepunguza mzigo wa kumeza idadi kubwa ya vidonge, lakini suala la kumeza dawa kila siku bado ni changamoto katika matibabu ya Ukimwi. 
Miongoni mwa changamoto kubwa zinazoambatana na kumeza vidonge kila siku ni pamoja na kusahau, kushindwa kumeza dawa kutokana na maudhi ya dawa, kukwepa hali ya unyanyapaa au kushindwa kumeza pale mgonjwa anapokabiliwa na tatizo la kutapika.
Hali hii mbali na kuwa mzigo kwa wagonjwa, lakini pia inaathiri ufuasi mzuri wa dawa kwa baadhi ya watu.
Ni ukweli usiopingika kuwa, ufuasi mbaya na matumizi ya dawa za ARV yasiyozingatia kanuni na maelekezo sahihi ya wataalamu wa tiba kwa sababu yoyote ile, yanaambatana na hatari ya kusababisha usugu wa virusi vya Ukimwi dhidi ya dawa.
Lakini pia, hali hii inachangia wagonjwa wengi kushindwa kupata nafuu hata kama wanaendelea na matibabu.
Wanasayansi kwa muda mrefu sasa, wamekuwa wakitafuta njia mbadala ya kupunguza idadi ya vidonge au kuachana na matibabu ya kumeza kila siku.
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa katika siku za usoni, matibabu ya Ukimwi hayatategemea tena umezaji wa vidonge kila siku na badala yake wagonjwa wataanza kutumia dawa kwa njia ya sindano.     
Sindano za ARV zitapunguza au kuondosha changamoto na hofu ya watu kushindwa au kusahau dozi ya kila siku ya ARV. Sindano hizi kwa mujibu wa watafiti zitakuwa zinatolewa mara moja kwa mwezi au kila baada ya miezi mitatu.
Wanasayansi wa kampuni ya kutengeneza dawa ya GlaxoSmithKline ya Marekani kwa kushirikiana na wale wa kampuni ya Janssen ya Ubeligiji, mwaka 2013 aliripoti kuwa hatua ya kwanza na ya pili ya majaribio ya dawa za ARV kwa njia ya sindano kwa binadamu, yameonyesha mafanikio na usalama mkubwa. Watafiti wa maswala ya dawa za ARV katika kitivo cha Afya ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Columbia Marekani, nao wanakiri kuwa ARV za sindano zina uwezo mkubwa wa kukabiliana na VVU.
Kwa sasa kampuni za ViiV Healthcare na Janssen yanaendelea na mikakati ya kufanya majaribio ya dawa hizi katika hatua ya tatu ya majaribio. kampuni hizo zinatazamia kuanza majaribio ya hatua ya tatu mwaka huu.
Wataalamu wa maswala ya utabibu wanaamini kuwa hii itakuwa hatua muhimu katika jitihada za kuboresha tiba ya Ukimwi duniani.
Hata hivyo, wataalamu wanadai kuwa, watu watakaotumia ARV za sindano ni wale ambao watakuwa wametumia kwanza dawa za vidonge na kupunguza kwa kiwango kikubwa wingi wa virusi katika damu yao.
Dk Dominique Limet ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya ViiV Healthcare, anasema: “Ikiwa jaribio hili litafanikiwa, watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ambao kiwango cha virusi ndani ya damu yao ni cha chini, watapata njia mbadala ya kutumia sindano.”
Wataalamu pia wanasema kuwa, ARV za sindano zinaweza kuwa na manufaa pale zitakapotumika kama kinga kwa watu walioko kwenye mazingira yanayoongeza hatari ya maambukizi ya VVU, ikiwa ni pamoja na wanandoa wenye hali tofauti za maambukizi.
Kutokana na ukweli kwamba ARV za sindano zinalenga watu ambao wametumia kwanza vidonge na kudhibiti virusi kwa ufanisi, wagonjwa ambao ufuatiliaji wa matibabu yao si mzuri, kwa maana ya kutotumia dawa kikamilifu, wanaweza kushindwa kufaidika na maendeleo ya kisayansi ya ugunduzi mpya wa njia ya kutumia ARV za sindano.
Uzuri wa ARV kwa njia ya sindano ni kwamba haina usumbufu na maudhi mengi ikilinganishwa na kumeza vidonge kila siku.
Pamoja na mafanikio haya ya kisayansi katika tiba ya Ukimwi, baadhi ya wanasayansi wana wasiwasi kuhusu ufanisi wa tiba hii hasa linapokuja swala la mtu kupata mzio wa dawa.
Dk Paul E. Sax, profesa wa maswala ya tiba katika Chuo Kikuu cha Harvard anasema kuwa, kama itatokea mtu akaanzishiwa dawa hii ya sindano ambayo inakaa mwilini kwa zaidi ya mwezi na ikamsababishia madhara kama vile mzio, dawa hii itasababisha mateso makubwa kwa mgonjwa.
Wachunguzi wengine wa mambo wanadai kuwa, madhara mengine ya ARV za sindano yanaweza kuwa ni kutokea kwa usugu wa virusi dhidi ya dawa kwa watu ambao watashindwa kupata dozi kwa wakati kama wanavyopangiwa.
Hata hivyo wataalamu wengi wanaamini kuwa ARV za sindano zinazotolewa mara moja kila mwezi au mara moja kila baada ya miezi mitatu, zitapunguza kwa kiwango kikubwa changamoto na adha kwa watu ambao walikuwa wanapata maudhi kwa kumeza vidonge vingi kila siku.
Wengi wanaamini kuwa njia hii ya kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, itasaidia kwa kiwango kikubwa idadi ya watu wanaoshindwa kufuatilia na kutumia vizuri dawa zao na itaboresha maisha ya wagonjwa wengi wenye tatizo la upungufu wa kinga mwilini.     

No comments:

Post a Comment