Tuesday 15 March 2016

LEO NI MAADHIMISHO YA SIKU YA UTEPE MWEUPE DUNIANI. MARCH 15.


Watanzania leo wanaungana na watu wote duniani katika kuadhimisha siku ya utepe mweupe (white ribbon) unaoadhimishwa kuchochea uzazi salama kwa wanawake wote duniani.
Idadi kubwa ya wanawake duniani kote wanakufa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi; inakisiwa kwamba hapa nchini kiasi cha wanawake 8,000 kila mwaka hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi. Idadi hii ya watu ni kubwa kwa viwango vyovyote vile; vifo hivi vina madhara makubwa kijamii na kiuchumi.


Wanaokufa ni nguvukazi ya taifa, lakini pia vifo hivyo mara nyingi vimechangia kuacha watoto yatima nyuma ambao wameleta changamoto kubwa kwa jamii katika malezi kwani anapokufa mzazi mmoja katika familia mtikisiko unakuwa mkubwa, aghalab familia nyingi husambaratika.
Inakisiwa kuwa zaidi ya wanawake 450 hufa  kila mwaka kati ya wanawake 100,000 wanaojifungua nchini. Sababu za vifo hivi zinaelezwa kuwa ni uzazi, ijapokuwa kimsingi uzazi si sababu hasa ila uduni wa huduma za afya za uzazi ndizo zimekuwa kikwazo kikubwa
.
Mara nyingi vifo hivi ingawa vinatokea pia katika hospitali wakati wa kujifungua na hata baada ya kujifungua, utaratibu wa kujifungulia nyumbani, kukosekana kwa huduma bora ya ukunga, umbali wa vituo vya afya na gharama zinazoambatana na huduma hizo, kwa ujumla wake ni mambo ambayo yanatajwa kuwa vikwazo cha kufikiwa kwa uzazi salama nchini.

Kwa sasa Tanzania inatajwa kushika nafasi ya tano katika nchi zenye hali mbaya zaidi ya vifo vinavyotokana na uzazi, hali hii kwa ujumla inaonyesha kwamba kama taifa kuna changamoto kubwa ya kufikiwa kwa malengo ya milenia hasa hali ya nafasi ya wanawake kwa ujumla inapoangaziwa.Uzazi salama umekumbwa pia na changamoto za mila na desturi potofu ndani ya jamii, miongoni mwake ni kuwanyima elimu watoto wa kike, kuwaozesha mabinti katika umri mdogo, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake kama vile ukeketaji, kupigwa na mambo mengine yanayowaletea msongo na hivyo kujikuta wakipatwa na maradhi kama vile shinikizo na majonzi katika maisha.

Kuwanyima wanawake fursa za kumiliki uchumi, kama vile mila potofu za kuwakatalia kumiliki ardhi, kukataliwa kufanya kazi za kuwapatia kipato na hata katika shughuli za kilimo kushindwa kuwa na maamuzi juu ya kile walichozalisha, kumewafanya wanawake washindwe kufikia huduma bora za afya wakati wanazihitaji, hususani wakati wa kujifungua na mwishowe huishia kuhudumiwa na wakunga wa jadi ambao hawawezi kuhimili matatizo makubwa ya uzazi yanapojitokeza.

Uhuru wa kiuchumi kwa wanawake unaweza kuwa moja ya ufumbuzi wa kupunguza matatizo ya uzazi kama watakuwa na maamuzi juu ya mali ambazo ama walishiriki kuzizalisha au hata kama zinamilikiwa na familia kwa pamoja. Ni jambo lisiloeleweka katika jamii iliyogubikwa na mfumo dume eti mali ya familia iuzwe ili kuokoa maisha mama mjamzito anapokumbwa na matatizo ya uzazi.
Kwa ujumla wake, uzazi salama kwa Tanzania bado ni safari ndefu iliyojaa milima na mabonde mengi ambayo jamii ni lazima ijitazame kwa pamoja jinsi ya kukabiliana nayo kama kweli tunataka kuona hatua zikipigwa kupunguza vifo vya uzazi ambavyo vinazuilika.


Ni kwa maana hii tunachukua fursa hii kuikumbusha jamii yetu, tukigusa makundi mbalimbali ya kijamii, vyama vya kutetea haki za binadamu, vyombo vya serikali na kila mdau mwenye kuitakia jamii mema, kuitazama siku ya leo ya utepe mweupe kama tangazo la kukumbushana nini kifanyike kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya uzazi na wakati huo huo kuokoa maisha ya watoto  chini ya miaka mitano kwa nia ya kujenga jamii yenye siha zaidi itakayounganisha nguvu zake kuleta maendeleo ya taifa kwa umoja wake.

No comments:

Post a Comment