Saturday 26 March 2016

VYOMBO VYA HABARI NCHINI VYATAKIWA KUELIMISHA WANANCHI KUHUSU UGONJWA WA KIPINDUPINDU.


Vyombo vya habari vimetakiwa kuelimisha wananchi kuchukua tahadhari  ya ugonjwa wa kipindupindu ambao tangu uanze miezi saba iliyopita bado upo na unazidi kuenea na kusababisha vifo.


Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa ufatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko mkoani Dodoma, Bw. Gerald Manasseh wakati wa semina ya waandishi wa habari.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya chanzo cha ugonjwa, dalili, ueneaji wake, athari zake, jinsi ya kujikinga na namna ya kumhudumia mgonjwa wa kipindupindu.
Pia amesema katika wilaya za mkoa wa Dodoma wananchi walioathirika na ugonjwa huo asilimia kubwa ni wale wanaotumia maji kutoka vyanzo ambavyo  si rasmi.
Aidha ameongeza kuwa, kati ya machi 12 – 22 kulikuwa na wagonjwa wapya 92 wa kipindupindu huku wagonjwa watatu wakiwa wamefariki dunia, hata hivyo amesema kwa sasa wamebaki wagonjwa saba.
Semina hiyo iliyoendeshwa na shirika la afya duniani (WHO) kwa kushirikiana na hospitali ya mkoa na ofisi ya raisi tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) imevitaka vyombo vya habari kufanya kazi zake bila kujali vinalipwa nini ili kuutokomeza ugonjwa huo mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wake Afisa afya na mazingira kutoka TAMISEMI Bi.Stella Kajange amesema  ugonjwa wa kipindupindu uko mkoani Dodoma tangu agosti mwaka jana na sababu kubwa zinazofanya uendelee  kuenea ni uelewa mdogo  wa wananchi juu ya ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment