Tuesday 22 March 2016

MARCH 23 YA KILA MWAKA WATU WOTE DUNIANI HUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA.


Tarehe ya 23 Machi kila mwaka Shirika la Hali ya Hewa Duniani(WMO) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huadhimisha siku ya hali ya hewa Duniani. Maadhimisho haya ni kumbukumbu ya siku ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani tarehe 23 Machi,1950.



Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa sheria ya wakala wa serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi mwezi Desemba 1999. Mamlaka inafanya kazi zake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na inaiwakilisha  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirika hilo.

 Tanzania kupitia (TMA) inaadhimisha siku hii ya hali ya hewa duniani kwa kusherehekea mafanikio yaliyofikiwa na WMO tangu kuanzishwa kwake na Mafanikio ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini.

 Miongoni mwa majukumu ya TMA ni pamoja na kufanya shughuli za uangazi, kukusanya na kuhifadhi  data na takwimu za hali ya hewa, kutoa utabiri wa hali ya hewa na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini na nje ya nchi.

TMA pia inaiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kimataifa na  pia Mamlaka inashirikiana na wadau wengine hapa nchini na katika kanda ya Afrika mashariki na kusini mwa Afrika ili kuboresha utabiri wa hali ya hewa wa msimu ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tunaposherekea siku ya hali ya hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inajitahidi kutoa huduma za hali ya hewa za kuaminika, zinazotolewa kwa wakati, zenye viwango vya usahihi vinavyokubalika na katika lugha rahisi na ya kueleweka ili kukidhi mahitaji ya jamii ikiwa ni pamoja na watoa maamuzi na hivyo kuchangia katika maendeleo ya Taifa. Mfano mzuri wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa  katika kufanya maamuzi ni katika sekta ya kilimo na usafiri wa Anga.

Uelewa wa kuanza, kuisha na urefu wa msimu wa mvua ni muhimu katika kufanya maamuzi ya shughuli za kilimo kama vile, wakati gani wa kupanda na kuvuna, pia aina gani ya mazao yanaweza kupandwa , wakati gani wa kunyunyizia dawa na namna gani ya kuhifadhi mazao.  Katika Usafiri wa anga taarifa za hali ya hewa ni muhimu wakati wa kutua, kupaa na usafiri wa ndege inapokuwa angani. Aidha, taarifa za hali ya hewa zinatumika kibiashara na wamiliki wa ndege katika kujua kiasi cha mafuta yanayohitajika na kiasi cha mzigo unaoweza kubebwa katika safari husika.

Maeneo mengine ambayo taarifa za hali ya hewa ni za muhimu ni katika ujenzi, mipango miji pamoja na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi.  Taarifa za hali ya hewa husaidia wahandisi na maafisa mipango miji kuainisha maeneo ya kuweka miundombinu mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya maji safi na  maji taka, ujenzi wa  madaraja n.k.  Takwimu za vimbunga na mfumo wa upepo katika ukanda wa Pwani ni muhimu sana katika shughuli zinazoendelea za utafiti na uchimbaji wa mafuta. Idadi ya siku ambazo mvua itanyesha na hali ya joto ya mahali husika ni muhimu katika sekta ya utalii.

Taarifa za matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile mafuriko na ukame, upepo mkali pamoja na mvua ya mawe na kujua eneo litakalo athirika ni muhimu sana katika mipango mbalimbali ya maendeleo.
Hii ni baadhi ya mifano michache tu ambapo uhitaji na uelewa wa huduma za hali ya hewa hauepukiki. Katika kuhakikisha kuwa jamii yetu inafikiwa na huduma hizi muhimu za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) husambaza taarifa hizi kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kama vile, Facebook, Twitter, YouTube.

Kutokana na kuongezeka uelewa wa sayansi ya hali ya hewa, utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuongezeka viwango vya usahihi na hivyo nashauri sekta zote za kiuchumi na kijamii hapa nchini kuendelea kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa  katika kupanga mipango yao ya muda mfupi na mrefu.

 Endapo utabiri wa hali ya hewa utolewao na TMA utazingatiwa na kutumiwa kwa makini utasaidia sana katika kupunguza athari za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa Adha, ikumbukwe kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuokoa maisha na kupunguza hasara ya upotevu wa mali kwa kuwa na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa.

TMA imepata cheti cha ubora cha kimataifa (ISO 9001:2008) katika utoaji wa huduma  bora za hali ya hewa kwa usafiri wa anga. Cheti hiki kilipatikana mwaka 2011 na hii ni sifa kwa nchi yetu hasa ikikumbukwa kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kupata cheti hicho kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.  Mipango iko mbioni kuhakikisha huduma zitolewazo na TMA katika sekta zote zinasajiliwa na shirika la viwango duniani.  Hivyo tunaposherehekea siku ya hali ya hewa Duniani naendelea kuwashauri watanzania wenzangu katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kutumia taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.
 Nawatakia maadhimisho mema ya siku ya hali ya hewa duniani mwaka huu wa 2016.



No comments:

Post a Comment