Saturday 19 March 2016

AGIZO LA RAIS MAGUFULI JUU YA WACHEZA POOL NYAKATI ZA KAZI LAANZA KUTEKELEZWA MKOANI GEITA.


 Kamanda mkuu wa jeshi la polisi mkoa wa Geita , Mponjoli Mwabulambo
Agizo la Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr.John Pombe Magufuli la kupiga marufuku kucheza Pool nyakati za kazi  limeanza kutekelezwa mkoani Geita katika Wilaya ya Bukombe na kwamba  Jeshi la Polisi limewanasa na kuwatia mbaroni vijana 22 wakicheza mchezo huo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita kamishna msaidizi Mponjoli Mwabulambo amesema vijana hao walikamatwa jana katika msako mkali unaoendelea na  kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mponjoli amesema msako huo umelenga maeneo ya Stend za magari mjini ushirombo pamoja na kwenye nyumba za starehe yaani  Bar  na maeneo mengine ambayo huchezwa mchezo huo ambao serikali imeupiga marufuku kuchezwa nyakati za kazi.

Mwanzoni mwa wiki hii Rais Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wa Mikoa nchini alipiga marufuku mchezo wa Pool na kuwaagiza viongozi hao mikoani kuhakikisha wanawakamata wale wote watakaobainika wanacheza Pool wakati wa Kazi na sasa mchezo huo utachezwa kuanzia saa 10 jioni.

Aidha Mponjoli amesema msako huo utaendelea katika maeneo yote ya wilaya ya Bukombe ikiwemo kwenye miji yote yenye mikusanyiko ya watu hata vijiji ambako mchezo huo unachezwa nyakati za kazi hali itayofanya Agizo la Rais Magufuli la kila mtu kufanya kazi linatekelezwa .

Pia Mponjoli amewaonya vijana wote wanaojihusisha na Uharifu wa aina yoyote waache mara moja kabla ya kukamatwa kwani shughuli ya wizi huo katika awamu hii ya Tano haina nafasi na kuwataka wakafanye kazi zingine ambazo ni halali za kuwaingizia kipato.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukombe SP Leonard Nyandahu amesema wafanyabiashara wote wanaomiliki Pool katika miji ya Ushirombo na Runzewe,Uyovu wameziondoa Pool zote kwenye maeneo yao yote ya biashara zao.


Nyandahu amesema  kuwa katika msako wake wafanya biashara hao wengi wao wamefunga kabisa mchezo wa Pool kwenye maeneo yao ya Biashara kwa madai kuwa wanamuunga mkono Rais Magufuli ambaye katika agizo lake alisema mchezo huo uchezwe kuanzia saa 10 jioni lakini wao wamefuta kabisa katika maeneo yao kwani vibaka walikuwa wakitumia kufanya mipango yao ya uharifu.

No comments:

Post a Comment