Thursday 24 March 2016

MARCH 24 KILA MWAKA NI SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI.




Kifua Kikuu (TB) ni ugonjwa ambao unafahamka kwa watu wengi  katika Tanzania kutokana na madhara mengi ambayo yamejitokeza na kuonekana iwe katika familia au katika jamii kwa namna moja au nyingine.

Huu, ni ugonjwa ambao umedumu kwa karne nyingi tangu ulipogunduliwa na mtaalam kutoka Ujerumani, Dk Robert Koch mwaka 1882 na kuushangaza ulimwengu wa tiba kwa ugunduzi wake huo.
Mgunduzi wa Kifua Kikuu,  Robert Koch alipewa tuzo ya amani ya Nobel kwa ugunduzi wake huu ambao kwa kiasi kikubwa umeiokoa dunia.

Kwa nyakati tofauti, walimwengu wakiwamo wanasayansi walikaa na kukubaliana  kuanzisha Siku  ya Kifua Kikuu duniani itayoadhimishwa kila siku ya Machi 24 kila mwaka.
Siku hiyo ni mahsusi  kwa ajili ya kufanya mapitio kuhusu hali halisi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kwa hiyo, siku hiyo ya ugunduzi wa Dk Koch hadi sasa  imekuwa ikiadhimishwa kote duniani kila mwaka na kwa mwaka huu ikiwa na kauli mbiu, ‘Tuungane kutokomeza  Kifua kikuu`
Inaelezwa kuwa mtu menye vijidudu vya ugonjwa huo akihoa, kupiga chafya au kwa namna yoyote nyingine kurusha vitone vya makohozi yake kutoka katika mfumo wake wa hewa na kuvieneza hewani na mtu mwingine kumpata akivuta hewa ndani na hivyo kuingia katika mfumo wa hewa.
Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea kwa  kiasi kikubwa na kuwapata watu masikini  zaidi .
Vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka katika Tanzania.
Kulingana na WHO, Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa na ugonjwa huu barani Afrika.
Kati ya asilimia 50 ya wagonjwa wa Kifua Kikuu waliopimwa virusi vya Ukimwi mwaka 2007, inakadiriwa kuwa asilimia 47 walikuwa pia na virusi vya Ukimwi.
Ugonjwa  huu husababishwa na bakteria waitwao,  Mycobacteria tuberculosis.

Aina hii ya bakteria huathiri mapafu, tezi (lymph nodes), tumbo na sehemu nyingine za mwili.
Wataalam wanaeleza kuwa asilimia 10 tu ya watu walio na bakteria hao jamii ya Mycobacteria tuberculosis hawapati ugonjwa huu wa Kifua Kikuu.
Ø  Aina za Kifua Kikuu
Kuna aina kuu tatu za ugonjwa wa Kifua Kikuu;
-Kifua kikuu kinachosababisha madhara (active tuberculosis) – hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa bakteria wasisababishe madhara. Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yoyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu.
-Ugonjwa usiosababisha madhara (inactive tuberculosis) – Kwa kitaalamu huu pia huitwa Latent TB. Hapa inaamaanisha kuwa kinga ya mwili imeweza kuwadhibiti bakteria na kuwafanya kushindwa kusababisha madhara.
Mtu mwenye Latent TB, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu.
Aina hii inaweza kujirudia baadaye na kuathri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadaye huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.
-Ugonjwa uliosambaa mwilini (milliary tuberculosis) – Hii hutokea pale ambapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo (pericadium), mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.
Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.
Vihatarishi vya ugonjwa wa Kifua Kikuu
Ø  Vihatarishi vya ugonjwa huu ni;
-Uzee
-Unywaji pombe kupindukia
-Kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi, hospitali, mabasi ya abiria.
-Magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari.
-Wafanyakazi wa huduma ya afya
-Ugonjwa wa Ukimwi
-Utapiamlo
-Umaskini au hali duni ya kipato
-Kuishi kwenye nyumba za jamii, mfano nyumba za wazee
-Wale wasio na makazi
-Baadhi ya dawa – Dawa za ugonjwa wa maumivu ya mifupa (athritis)
-Wasafiri au watalii kutoka nchi zilizo na idadi kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Ø  Dalili na viashiria vya ugonjwa wa Kifua Kikuu
-Kukohoa zaidi ya wiki 2-3 na kuongezeka kutoa makohozi
-Kukohoa damu
-Homa za mara kwa mara
-Kupungua au kukosa hamu ya kula
-Kupungua uzito kwa asilimia 10.
-Kutokwa na jasho kwa wingi hasa wakati wa usiku
-Uchovu
-Maumivu makali ya kichwa
-Maumivu ya kifua
-Kupumua kwa shida
Vipimo vya Kifua Kikuu
-Kipimo cha makohozi (Sputum for AFB) – Makohozi huchukuliwa kwa siku tatu mfululizo muda wa asubuhi na kupelekwa maabara kufanyiwa uchunguzi ili kuweza kugundua kama mtu ana TB.
Kwa wale wagonjwa wasioweza kutoa makohozi au wale wenye TB ya tumbo, basi hufanyiwa kipimo cha gastric lava.
                    KWA PAMOJA TUUNGANE KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU. 8

No comments:

Post a Comment