Monday 30 January 2017

WALIMU SHULE YA MSINGI ISABILO WAGOMA KUFANYA KAZI



Walimu  wa shule ya msingi Isabilo wilaya na Mkoa wa Geita wamegoma kufanya kazi tangu Januari 25 mwaka huu  kutokana  na kile kinachodaiwa kuwa  ni kukosa  morali ya kazi baada ya   wanakijiji kuvamia na kuwapiga walimu wawili kwa tuhuma za  kuwaadhibu watoto   wao.
Wakizungumza na Storm habari  wakati  wa ziara ya Katibu wa Chama cha walimu C.W.T  tawi la Geita  Mwl. John Kafimbi  walimu waliofanyiwa kitendo hicho Medard Zacharia na Deograsi  Ristone  wamesema  kitendo kilichofanywa  na wananchi kuwapiga walimu kimewafedhehesha  sana.

Kaimu mkuu  wa shule ya msingi  Isabilo mwl. Athuman Augustine amesema sababu ya kuadhibiwa  kwa wanafunzi  ni kutokana na kutokufika shuleni hali ambayo iliwapelekea kuwapa adhabu ya viboko vitatu kwa kila mwanafunzi ambaye hakuhudhuria siku ya usafi shuleni wakati wa likizo.

Katibu  wa Chama cha Walimu  Wilayani Geita John Kafimbi  amesema  kuwa suala hilo  halitavumiliwa kuona walimu wanadhalilishwa na kwamba hatua kali zichukuliwe na Serikali dhidi ya wananchi ambao wametenda kitendo hicho.

Pia imeelezwa kuwa wakati walimu hao wakitoa adhabu  mmoja wa wanafunzi hao  anayesumbuliwa na mapepo alianguka na kuzimia hali iliyopelekea wazazi kuwa na jazba  kisha kuhamasisha wananchi kuvamia shuleni hapo.                

No comments:

Post a Comment