Watoto wanne wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketea kwa moto
walipokuwa wamelala chumbani katika tukio lililotokea mtaa wa Geita Road Kata
ya Nyatukala mjini Sengerema mkoani Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amesema tukio hilo lilitokea
saa tano usiku wa Februari 28, 2018 na kuwataja watoto hao kuwa ni Redia Elias
(10), Modesta Elias (9), Steven Deogratias (9), na Kizengela Elias mwenye umri
wa miaka ninane.
Amesema wakati moto huo uliotokana na mshumaa kushika chandarua na
kuunguza godoro walilokuwa wamelalia, mama yao alikuwa amelala kwenye nyumba
nyingine ya familia hiyo.
“Watoto wote ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Pambalu na wanatarajiwa
kuzikwa kesho,” alisema Kipole.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Amas Juma amewataka wazazi kuwa makini
pale wanapolazimika kuwawashia watoto mishumaa kwa kuhakikisha inazimwa kabla
ya kulala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema polisi wanaendelea
na uchunguzi kuhusu tukio hilo na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua
tahadhari watoto wanapobaki wenyewe nyumbani.
No comments:
Post a Comment