Monday, 12 March 2018

WANANCHI WAVAMIA KITUO CHA POLISI JAMII NA KUHARIBU MIUNDOMBINU HUKU WAKIKWAMA KUKICHOMA MOTO

Jengo ambalo lilikuwa likitumika kama ofisi za Polisi Jamii kwenye Mtaa wa Nyakabale Kata ya Mgusu likiwe limeharibiwa na kuvunjwa vioo na baadhi ya wananchi kutokana na kuchukizwa kwa kitendo cha kuadhibiwa Mmoja kati ya wananchi wa mtaa huo na Kikosi cha Polisi Jamii.

Baadhi ya Nyaraka zikiwa zimechomwa Moto ndani ya Ofisi za Polisi Jamii mtaa wa Nyakabale Wilayani Geita.

Kiongozi wa polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale Bw Nyeresi Charles,akielezea namna tukio lilivyoweza kutokea na wananchi kufikia hatua ya kuvamia ofisi zao.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Geita ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Mwl Herman Kapufi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuona uharibifu kwenye kituo hicho. 

Bomba la maji likiwa limekatwa na baadhi ya wananchi ambao walivamia kwenye kituo cha Polisi Jamii.


Katika hali isiyo ya kawaida Wananchi wa mtaa wa Nyakabale na Manga kwenye Halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita wamekivamia na kuharibu miundombinu ya kituo cha polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale huku jaribio la kukiteketeza kwa moto  kituo hicho likishindikana.

Tukio hilo limetokea jana jumapili majira ya asubuhi ambapo inadaiwa kuwa kundi la watu zaidi ya 200 limevamia kituo hicho kwa madai ya kulipiza kisasi kutokana na mwenzao aliyetambulika kwa jina la Zakaria Shaban (36) kudaiwa kupigwa na polisi jamii  ambao ni walinzi wa mgodi wa dhahabu wa Geita, GGM hadi kufa.

Hata hivyo kiongozi wa polisi jamii katika mtaa wa Nyakabale Bw Nyeresi Charles amesema mtu huyo ambaye inadaiwa ameuawa na Polisi jamii, inasadikika kuwa alipigiwa mgodini Tarehe 7 mwezi huu na kwamba wanashangaa kuona wananchi wamekwenda kwenye ofisi zao na kufanya uhalifu kwa kuharibu baadhi ya vitu huku wakijaribu kutaka kuchoma Jengo ambalo limekuwa likitumika.

Mwenyekiti wa mtaa wa Manga   Bw Mtedi Lukanya  alisema  hakuna mwenye uhakika wa mtu kufa na kwamba kama alipigwa tarehe 7 mwezi huu hapo katikati kumetokea jambo gani hadi kufanya uharibifu wa kuvamia ofisi siku ya Jumapili.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Geita ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Mwl Herman Kapufi amekiri kutokea kwa tukio hilo huku akiwasisitiza wananchi kuachana na desturi ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba kama kuna tatizo ni bora wavishirikishe vyombo vya dola na kama vinashindwa ni bora wakawasiliana naye moja kwa moja.

Jeshi la polisi wilaya ya Geita limefika katika mtaa huo na kuwakamata watu wanne wakiwemo wanawake wawili na wanaume wawili na bado linaendelea na uchunguzi kuwabaini wengine wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment