Friday 16 March 2018

WANAODHOROTESHA ZAO LA PAMBA KUCHUKULIWA HATUA KALI ZA KINIDHAMU GEITA

Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi akizungumza na wadau wa sekta ya pamba kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkoa huo.
Wakuu wa Wilaya za Mbongwe,Chato na Bukombe wakimsiliza Mkuu wa Mkoa wakati wa kikao cha wadau wa Sekta ya pamba mkoani Geita.
Katibu tawala msaidizi idara ya uchumi na uzalishaji mkoani humo Emily Kasagara,akielezea mikakati ya utekelezaji wa kilimo cha pamba Mkoani Geita.
Meza kuu ikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi,Katibu wa chama cha mapinduzi Mkoani humo,Adam Ngarawa na Mkuu wa Wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi wakati wa kikao cha wadau wa sekta ya zao la Pamba.
Wenyeviti wa Halmashauri za Geita Mji,Geita DC,Mbongwe na Bukombe wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Katibu tawala msaidizi idara ya uchumi na uzalishaji mkoani humo Emily Kasagara.


Wakati  serikali  Mkoani Geita ikiendelea kujidhatiti vyema kurudisha hadhi ya kilimo cha pamba  Imebainika  kuna watu wachache ambao wameendelea kuzorotesha jitihada za kilimo cha zao hilo la biashara  kutokana na  baadhi ya wataalamu kuchukua dawa za viuwatirifu na kuzipeleka kwenye maduka ya kilimo  kwa ajili ya kuuzwa kwa Bei kubwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi wakati wa kikao  cha wadau wa kilimo cha pamba  mkoani humo ambacho kilikuwa kimelenga kutathimini usambazaji wa viuwadudu pamoja na maandalizi ya soko  la msimu wa pamba ambalo linaanza  mwezi mei. Ambapo alisema Serikali haiwezi kuwavumilia watu ambao wamekuwa wakirudisha nyuma jitihada za ulimaji wa zao hilo.

“Kuna watu wachache ambao hawana nia njema na mpango huu dawa zinaweza zikapotea njiani zikaingia bahati mbaya kwenye maduka ya jumla na mtumishi yoyote tutakaye mkamata hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa mara moja serikali imewekeza fedha nyingi  na hivi viuadudu ni vidogo tu lakini kwa sababu ya tamaa baadhi ya watu wamekuwa wakivipeleka kwenye maduka ili viuzwe bei ghali tutaanza kufanya uhakiki wa haraka” Alisisitiza Luhumbi.

Luhumbi ameongeza kwa kuwataka wakulima kuondokana na dhana ya kuweka fedha ndani na badala yake watumie asasi za kifedha yakiwemo mabenki kuweka  fedha zao kwani kufanya hivyo itawasaidia kuweka sehemu salama na kuepukana na vitendo vya kuendelea kuibiwa pindi wanapokuwa wameuza mazao yao.

Aidha Samweli Shangembe ambaye ni Mkulima wa pamba Wilayani Chato  ,alisema utaratibu ambao umewekwa wa kufungua akaunti ni mzuri ila ameiomba serikali kutoa waraka kwenye uongozi wa vijiji ili waweze kuwahamasisha wakulima wote ambao wamelima zao la pamba waweze kufungua akaunti.

Kwa upande wake Katibu tawala msaidizi idara ya uchumi na uzalishaji mkoani humo Emily Kasagara alisema Katika msimu wa kilimo 2017/18 Mkoa ulilenga kulima hekta elfu sabini na nane miatano arobaini  na tisa (78,549) ambazo ni sawa na ekari laki moja tisini na sita elfu miatatu sabini na tatu ( 196,373)  ambazo zinatarajia kutoa mavuno ya tani elfu tisini na nane mia moja tisini na sita nukta tano  (98,196.5.)

“Hadi Desemba .2017 jumla ya wakulima elfu sabini na nne mianane arobaini na sita (74,846) walikuwa wamejiorodhesha kulima zao la pamba,Hadi tarehe 15,Januari,2018 jumla ya ekari laki  mbili arobaini na moja elfu na arobaini  na tatu (241,043) sawa na hekta elfu tisini na sita mianne kumi  na saba (96,417) zilikuwa zimelimwa na kupandwa,Matarajio ya mavuno ni kati ya tani elfu sabini na mbili miatatu kumi na mbili nukta tisa (72,312.9) na  laki moja ishirini  elfu na miatano ishirini  na moja (120,521) kwa wastani wa uzalishaji wa kati ya kilo miatatu (300) kwa ekari” Alisema Kasagara.

No comments:

Post a Comment